Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Mawaziri waliotamba mwaka 2016

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage  

Dar es Salaam. Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano wamemaliza kipindi cha mwaka mmoja kinachostahili kutathmini utekelezaji wao wa kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” katika kutatua kero za wananchi.

Rais John Magufuli aliwateua mawaziri 18 na manaibu 19 Desemba 10 mwaka jana, akisema: “Niliowachagua wote ni wana CCM na wengi wao ni wabunge. Waliinadi sera ya “Hapa Kazi Tu” na ndiyo maana hakuna haja ya semina elekezi. Spidi ni hiyohiyo, ndiyo maana hatutatumia semina elekezi ya bilioni mbili.”

Mwananchi imetafuta maoni ya wananchi mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa mawaziri hao katika kipindi cha mwaka mmoja.

Bila ya semina elekezi, mawaziri hao wamewajibika kila mtu kwa staili yake, kitu ambacho kimewafanya wasomi, wachambuzi na wananchi kuwatofautisha wale ambao staili zao ziliwakuna tofauti na wengine.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametajwa zaidi katika kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi hasa migogoro ya ardhi.

Mwingine ni Angella Kairuki (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Umma,) aliyetajwa kulifanyia kazi kwa kina suala la watumishi hewa na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani) aliyesifiwa kwa tabia yake ya kutatua kero papo kwa papo.

Pia katika orodha hiyo yumo Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) ambaye ametajwa kutokana na kushughulikia suala la upatikanaji wa umeme.

Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye amesifiwa kutokana na jitihada zinazoendelea za kuboresha usafiri na harakati zake za kutembelea maeneo mengi, hali kadhalika, Charles Mwijage kutokana na kazi aliyofanya ya kuelewesha dhana ya viwanda.

Lukuvi awakuna wengi

Lukuvi ndiye aliyeongoza orodha ya mawaziri waliovutia wengi.

“Ameonyesha wazi kukerwa na dhuluma wanazofanyiwa wananchi wa chini katika masuala ya ardhi,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) mkoani Morogoro, Mwadhini Muyanza.

Kauli kama hiyo alitoa mkazi wa Mji Mpya mkoani Dodoma, Jella Mambo ambaye alisema Lukuvi ameonekana kujitahidi katika kutatua changamoto kubwa ya ardhi kwa wananchi wengi.

“Huyu ndiye waziri pekee ambaye tumemuona anafanya kazi ya utatuzi wa migogoro mikubwa ya ardhi kwa kuchukua hatua tofauti na mawaziri waliopita wa ardhi,” alisema mkazi mwingine wa mkoani Dodoma, Amina Godfrey akiungana na Mambo.

Kati ya watu saba waliohojiwa na Mwananchi mkoani Kilimanjaro, watano walisema kuwa wizara iliyoonekana kugusa hisia za walio wengi ni ile inayoongozwa na Lukuvi.

Walisema wizara hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zilizokuwa zikijirudia mara kwa mara, hasa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kiwanja kimoja kumilikiwa na watu watatu hadi wanne.

Walisema mabaraza ya ardhi yamepewa nguvu ya kutatua migogoro ya ardhi tofauti na awali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Danford Kitwana alisema awali kulikuwa na migogoro mingi iliyosababishwa na viongozi hao kutokuwa karibu na wananchi kusikiliza kero, hali iliyosababisha migogoro.

“Lukuvi amejitahidi sana kuwa karibu na wananchi kutatua kero zinazowakabili na kwa sasa vilio vya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi vimepungua. Nampongeza ila azidi kupambana,” alisema Kitwana.

Innocent Lema, anayejihusisha na biashara ya nguo jijini Mwanza, alisema kwa kipindi kirefu Wizara ya Ardhi imegubikwa na matatizo, lakini Lukuvi ameyashughulikia kwa asilimia zaidi ya 60.

“Mawaziri wengi wamefanya kazi nzuri lakini Lukuvi amefanya kazi kubwa na ametatua changamoto nyingi zinazohusiana na ardhi kwa muda mfupi,” alisema Lema.

“Hakuna asiyejua kwamba migogoro ya ardhi ilikuwa tatizo kubwa kwa wananchi wengi, lakini tumeona anazunguka nchi nzima, anakaa na wananchi. Wanatoa kero zao, na si tu wanatoa kero halafu anatoa ahadi za kushughulikia, bali nyingi anazitatua pale pale.”

Wakati sifa zikimiminikia Lukuvi, mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo nchini, Johnson Minja aliitaja Wizara ya Nishati na Madini kuwa imeboresha upatikanaji wa umeme nchini na kumsifu Profesa Muhongo.

“Iilifikia mahali pa kuitwa ‘Tanzania ya giza’ kutokana na kutopatikana kwa umeme wa uhakika,” alisema Minja ambaye alimtaja Waziri Muhongo kuwa ndiye aliyehakikisha kuna umeme wa uhakika.

“Umeme kwa sasa umekuwa wa kudumu. Hakuna kukatikakatika. Kiukweli tumejionea tofauti katika wizara hii na tunapenda iendelee hivihivi katika utendaji wake,” alisema Minja.

Kadhalika, mchezaji wa zamani wa klabu ya Young Africans (Yanga), Ali Mayai Tembele alisema Wizara ya Nishati imeweza kubadilisha mfumo wa upatikanaji wa umeme tofauti na miaka kadhaa ya nyuma wakati nishati hiyo ilipokuwa inapatikana kwa shida.

Waziri Kairuki pia aliingia kwenye orodha hiyo akianza kutajwa na mkazi wa Dar es Salaam, Maliki Malupu aliyemsifu kuwa amefanikisha harakati za ofisi yake katika kuwashughulikia watumishi hewa kama alivyoagizwa na Rais Magufuli.

“Waziri Kairuki hakuishia tu kupambana na watumishi hewa, bali amekwenda mbali zaidi kukagua uhalali wa vyeti vya watumishi ili kila mmoja alipwe anachostahili,” alisema

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Rashda Masemela aliongezea suala la kushughulikia wafaidika hewa wa mradi wa Tasaf kuwa limemuongezea sifa.

Hata hivyo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Losolutie, pamoja na kusifu mawaziri kwa ujumla, alisema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeshindwa kutoa ajira kwa wananchi na kupandisha mishahara.

Mwigulu hasubiri taarifa

Mmoja wa askari mwenye Cheo cha Koplo ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ameshugulikia kero bila ya kusubiria taarifa zifikishwe ofisini kwake.

Alisema kitendo cha waziri huyo kukataza kununuliwa viatu vya askari wa Jeshi la Polisi na Magereza nje ya nchi ili kukuza soko la ndani ni kitendo cha kizalendo ambacho kinafaa kuigwa na mawaziri wengine.

Waziri mwingine aliyetajwa kufanya kazi kwa nguvu akionekana kupita maeneo yote ya nchi ni Waziri Mbarawa.

Mmoja wa watu waliozungumzia waziri huyo wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano ni Seana Chuli wa Kinondoni ambaye alisema hata katika suala la ununuzi wa ndege Profesa Mbarawa ndiye ameshika usukani.

“Huyu baba anapita kila eneo, kila mkoa, leo yupo hapa kesho pale, anapambana na ufisadi au anahakikisha barabara zinajengwa na tenda zinaenda sawa,” alisema.

Hata suala la kuondoa watumishi waliokuwa wakiharibu Shirika la Ndege (ATCL), kampuni ya simu ya TTCL na pia ujenzi wa barabara limehusishwa na waziri Mbarawa, kwa mujibu wa Anna Kasembe ambaye ni mkazi wa Masasi.

Katibu wa Chama cha Walimu jijini Mwanza, Asha Juma pia alimsifu Mbarawa akisema wizara yake imejitahidi kuhakikisha wananchi hawasumbuliwi na gharama za usafiri na kusafirisha mizigo.

“Tunaona Wizara ya Usafirishaji na Uchukuzi imejitahidi kuondoa adha ya usafiri na sasa wananchi wanaweza kutumia usafiri wowote tena kwa gharama nafuu. Pia imeweza kuleta ndege, inakarabati reli, pia na (inaboresha) usafiri wa majini,” alisema Juma.

Davis Daud ambaye alikuwa mwenyekiti wa vyama vya siasa visivyo na wabunge mkoani Mbeya, alisema mpaka sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imeongoza kwa kufanya vizuri akidai kuwa imeongeza njia za mapato na kuweka mazingira bora ya utalii nchini.

Davis alisema wizara hiyo ni moja ya wizara kubwa tano na kwamba imefanya mengi mazuri kuliko nyingine kwa kuongeza njia za mapato.

Wengine waliohojiwa na Mwananchi walimtaja Waziri Mwijage kuwa amefanya kazi kubwa kuelezea dhana ya uchumi wa viwanda, japo utekelezaji wake bado umekuwa mgumu kutokana na baadhi ya sheria na sera za viwanda kuwa ngumu kutekeleza.

“Dhana ya nchi ya viwanda imetangazwa na kuenea kila mahali, lakini kuna mlolongo wa kodi na utaratibu mrefu wa uanzishwaji wa hivi viwanda. Haya ni mambo ambayo yasipofanyiwa kazi yatamkwamisha Mwijage,” alisema Muyanza.

Lakini aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Njelu Kasaka alisema ni vigumu kutamka ni wizara gani imefanya vibaya au vizuri kwa sababu baadhi ya mawaziri wanafanya kazi kupitia vyombo vya habari, lakini wengine ni watendaji wa kimyakimya.

Alisema wapo mawaziri wanaofanya kazi kimyakimya lakini vizuri, huku wengine wanapiga kelele kwa kazi kidogo wanazofanya na kuonekana nchi nzima.

Kasaka alisema kwa msingi huo hana uhakika ni waziri yupi amefanya vema, lakini kinachoweza kutathiminiwa ni kwa kiasi gani wananchi wengi wamenufaika kwa kazi za mawaziri.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top