Dar es Salaam. Jaribio la kupinga hukumu ya kuwarejesha kazini wafanyakazi 31 waliopunguzwa mwaka 1993, limekwama tena baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya Benki Kuu Tanzania (BoT) ya kuongezewa muda wa kukata rufaa.
Nje ya Mahakama jana, wakili wa BoT, Sereni Mponda alisema anakusudia kuwasilisha rufaa kwa kutumia kipengele kingine akitaka mahakama ikubaliane na maombi yao ya kukata rufaa nje ya muda, akisema BoT ina nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa kuna suala aliloliita zito la kisheria linalohitaji mwongozo wa Mahakama ya Rufani.
Alidai Mahakama Kuu ilikosea kwa kuamini kuwa mkataba wa hiari uliotumika kuwapunguza wafanyakazi wote ulikuwa batili kwa sababu haukusajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Ajira.
Oktoba 2, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi ya BoT ya kuongezewa muda wa kukata rufaa kupinga uamuzi wa kuwarejesha kazini wafanyakazi hao ambao shauri lao limedumu kortini kwa miaka 22.
Lakini taasisi hiyo kuu ya fedha nchini ikaomba Mahakama ya Rufani irejee hukumu yake ya kutupa maombi yao ya kuongezewa muda wa kukata rufaa, ambayo jana yaligonga mwamba tena.
Watu hao 31 ni miongoni mwa wafanyakazi waliopunguzwa kazi na BoT mwaka 1993 wakati Serikali ikirekebisha uchumi, kwa kupunguza matumizi kulikoambatana na kupunguza watumishi, kazi ambayo Mahakama ilibaini ilifanywa bila ya kuzingatia sheria.
Akisikiliza maombi hayo jana, Jaji Semistodes Kaijage alitaka kufahamu kama kipengele cha 10 cha Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya 2000 kilichotumika kuyawasilisha kilikuwa kinaruhusu mahakama hiyo kusikiliza ombi hilo, lakini baada ya majadiliano na pande mbili, Wakili Mponda alikiri kuwa shauri hilo halifai kusikilizwa chini ya kifungu hicho.
Jaji Kaijage alisema ni lazima Mponda amridhishe kama kipengele cha sheria alichotumia kinawezesha mahakama kusikiliza ombi la kuongezewa muda ili BoT iweze kuwasilisha ombi la kuongezewa muda kuwasilisha taarifa ya kukata rufaa.
Wakili wa wafanyakazi 31 wa BoT, Barnaba Luguwa alimweleza Jaji Kaijage kuwa tatizo la upande wa BoT ni kung’ang’ania kanuni ya 10 badala ya kuangalia vipengele vingine vya sheria vinavyoweza kusaidia kumaliza mgogoro baina ya wateja wake na benki hiyo.
Loading...
Post a Comment