Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Waporaji 22 wa magari wakamatwa Dar

Kikosi  maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimewakamata watuhumiwa 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia kwenye mataa ya kuongozea magari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali zao kama simu za mikononi, kompyuta, saa na fedha.

Alisema ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti, ambapo Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko Magurumbasi na mataa ya Veta na Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi kutoka kwenye magari.

Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni Mtongani, Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi wa Keko Magurumbasi na wenzao saba.

“Katika mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.

Aidha alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka kusikojulikana. 

Wakati huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa makosa ya wizi kutoka kwenye magari.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli (21), Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed Idrisa(22) wote wakazi wa Keko na wenzao sita.

Katika tukio lingine, polisi wamewakamata watuhumiwa wanne wanaojihusisha na wizi kwa kuwarubuni watu kwa kukodi magari yao na baadaye hutumia nguvu  kuwapora.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Juma Kajeni (35), mkazi wa Tabata, Hamadi Kaganda (38), mkazi wa Mbagala, Mashaka Ally(62), mkazi wa Yombo na Mshamu Ally (32), mkazi wa Mtongani. 

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Pia aliwatahadharisha wananchi na wamiliki wa magari kuwa makini kwa watu hao ambao huja kwa nia ya kuwalipa fedha nyingi au kukodi gari kwa kiwango kikubwa na kisha wanatokomea na gari.

Wakati huo huo, polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na wizi wa magari kimekamata magari matatu ya wizi katika mikoa mbalimbali. 

Sirro alilitaja gari lenye namba T 386 CGY aina ya Verosa rangi nyeusi, mali ya Abraham Robert wa jijini Dar es Salaam na gari hilo lilikamatwa mkoani Mbeya likiwa limetelekezwa.

Gari jingine ni lenye namba T 946 DGH aina ya IST rangi ya fedha ikiwa inaendeshwa na mtuhumiwa aitwaye Hamadi Saidi (27) mkazi wa Kimara Dar es Salaam ambalo lilikamatwa huko mkoani Morogoro, gari hilo liliibiwa maeneo ya Kawe Beach jijini Dar es Salaam.

Alilitaja gari lingine kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba T 753 CVZ ambazo ni namba bandia huku namba zake halisi zikiwa ni T.815 DJF mali ya Magreth iliibiwa maeneo ya Kimara Suka jijini Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani. 

Pia alisema  watuhumiwa wengine waliohusika na wizi wa magari hayo wanaendelea kutafutwa ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari na watuhumiwa wengine wanaotafutwa kwa wizi wa magari hapo nyuma ambao walikimbia.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top