WAFANYAKAZI wanane wa kiwanda cha nondo cha Bansal kilichopo Kisongo wilayani Arumeru, Arusha, wameungua sehemu mbalimbali za miili yao baada ya uji wa chuma uliokuwa ukichemka kuwarukia.
Tukio hilo lilitokea jana kiwandani hapo na kuwasababishia wafanyakazi hao majeraha sehemu mbalimbali za miili yao ambapo walikimbizwa Hospitali ya Selian iliyopo jijini hapa.
Akizungumza jana hospitalini hapo, daktari aliyewahudumia wagonjwa hao, Rose Kaaya alisema aliwapokea majeruhi hao majira ya asubuhi kuanzia saa tatu ambao wameumia sehemu mbalimbali za miili yao huku wengine wakishonwa nyuzi kadhaa kwa sababu ya kuchanwa na vyuma wakati wakikimbia kujiokoa.
Dk Kaaya aliwataja majeruhi hao kuwa ni Hassan Guni (27), Christopher Semkiwa (24), Fred Sungi (21), Andrew Kihundwa (26), Calvin Langu (19), Simon Mkumbo (34), Simon Njuguna (25) na Tilak Tiwakraj (34), Mtanzania mwenye asili ya Asia.
Alisema majeruhi hao walipokewa hospitalini hapo na kutibiwa majeraha yao mbalimbali waliyoyapata kutokana na uji wa moto huo. Aliongeza kuwa, wameumia sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na nyuma ya shingo, mikononi na sehemu nyingine za miili yao.
Alisema majeruhi hao walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kisha kushauriwa kurudi leo hospitalini hapo kwa ajili ya kuangaliwa kwa ukaribu maendeleo ya vidonda vyao.
Mmoja wa majeruhi hao, Njuguna alisema awali asubuhi waliingia kazini kama kawaida, lakini baada ya muda waliona uji wa moto ukiruka na kuanza kuwaunguza kisha wao kukimbia ili kujiokoa.
“Hatujui chanzo cha kuruka kwa moto huu ila tumeungua sehemu mbalimbali za miili yetu na tunashukuru tumepata huduma za matibabu ila tumeungua,” alieleza.
Loading...
Post a Comment