Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Waziri Mbarawa atishwa na ufisadi wa meli, Mwanza

Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameahidi kubadili uongozi wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) katika vituo vya Kigoma na Mwanza kutokana na utendaji usioridhisha.

Profesa Mbarawa alisema hayo wakati akiwahutubia wafanyakazi wa Kampuni ya Ndege (ATCL), MSCL, Posta na Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani hapa.

“Haiwezekani meli ikatumia mtaji wa Sh3.6 milioni kufanya safari, halafu kilichopatikana ni Sh100,000. Hiyo ni biashara kichaa ambayo hakika siwezi kuivumilia hata kidogo,” alisema.

Waziri huyo alisema baada ya kupokea taarifa kutoka MSCL, amebaini kwamba kuna wafanyakazi wachache wasio waadilifu wala waaminifu ambao kwa muda mrefu wanatumia nyadhifa zao kujinufaisha na mapato yatokanayo na meli za Serikali na kusababisha wenzao kukosa mishahara kwa miezi 11.

“Nasema wapo watu nitawaondoa kwenye nafasi zao, kampuni ya Marine Services Limited na hata kuwahamishia maeneo mengine kwa sababu hawaendeni na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

“Ingawa pia nawataka wote mnaofanya kazi chini ya wizara yangu mbadilike kuanzia sasa,” alisema Profesa Mbarawa.

Ingawa hakutaja majina, Waziri Mbarawa alisema ataanza kuwaondoa wafanyakazi wanne ambao amejiridhisha kuwa utendaji wao hauridhishi.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alitaja hadharani namba yake ya simu ili kuongeza wigo wa kupokea malalamiko na kero kutoka kwa wafanyakazi waliopo chini ya wizara yake.

“Ninatoa namba ya simu yangu ya mkononi ili tuwe tunawasiliana kwa mambo ambayo yanahitaji ufuatiliaji na utekelezwaji, ingawa sipendi mnitumie taarifa zenye majungu. Hata hivyo, sipendi kuandikiwa sms za kuniomba michango kwa ajili ya harusi,” alifafanua.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa watumishi wa Tanroads, Ujenzi na Mawasiliano kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, Mongella aliungana na Mbarawa kuwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kufanya kazi kuzingatia sheria, kanuni na maadili.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top