NAIBU Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Athuman Mbuttuka amesema kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wabunge kuelewa kilichoandikwa kwenye ripoti ya CAG kutokana na lugha inayotumika kuhusisha maneno ya kitaalamu.
Alisema hayo jana wakati wa mafunzo ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambapo mada kuu ilikuwa uhusiano kati ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG), PAC na LAAC katika kuimarisha uwajibikaji sekta ya umma.
Alisema kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uandishi wa ripoti ya CAG unaohusisha maeneo ya kitaalamu ambayo yanakuwa changamoto kueleweka kirahisi kwa wajumbe.
“Wakati mwingine Kamati za Bunge hutumia ripoti ya CAG katika kujijenga kisiasa badala ya kuimarisha uwajibikaji,” alisema.
Pia alisema kumekuwa na changamoto ya wajumbe wa kamati kubadilika mara kwa mara na kutotekelezwa kwa maagizo yanayotolewa pamoja na kalenda ya ukaguzi kuingiliana na kalenda ya vikao vya Bunge.
“Uhaba wa muda na raslimali fedha kunapelekea PAC na LAAC kushindwa kupitia taarifa za CAG kwa mujibu wa kalenda,” alisema.
Alisema utendaji kazi wa CAG na mawanda ya ukaguzi wake yana uhusiano wa karibu na utendaji wa kazi wa kamati za hesabu za bunge katika kusimamia uwajibikaji katika sekta ya umma, hivyo uhuru wa CAG kifedha na kitaalamu ni muhimu katika kutekeleza matakwa ya kikatiba na kamati.
“Kamati zimepewa jukumu la kuisimamia na kuhakikisha kuwa serikali inawajibika kwa wananchi juu ya dhamana iliyopewa katika kusimamia na kutumia raslimali za umma, uhusiano huu unatengeneza mazingira ya kutegemeana ili kuleta uwajibikaji wenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Abdalah Chikota alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai amekuwa akibadilisha kamati kila baada ya miaka miwili lakini kwa mapendekezo yaliyofanywa na Bunge la Afrika Mashariki angalau wajumbe wa kamati wawe hata kwa miaka mitano kwani watakuwa na uwezo mpana wa kuhoji.
“Kuwa kwenye kamati ni mafunzo na mafunzo ni gharama kunahitaji uwekezaji mkubwa katika kuwapa mafunzo wajumbe,” alisema.
Alisema kikubwa kinachoangaliwa ni sheria ya bajeti ofisi ya CAG ikiandaa ripoti lakini isipopata fedha za kutosha hata kamati haziwezi kufanya kazi. Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Katavi, Rhoda Kumchele alisema kumekuwa na tatizo la ripoti ya CAG kujadiliwa kwa muda mfupi.
Loading...
Post a Comment