Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Ziara ya Rais Magufuli Kagera yatumbua watatu

Baada  ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza watumishi wote wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera waliohusika katika ukarabati wa majengo ya Shule ya Sekondari Omumwani ambayo yameonekana kutoendana na thamani ya fedha zilizotumika wachunguzwe, watumishi watatu wa manispaa hiyo wamesimamishwa kazi.

Watumishi hao walisimamishwa jana na Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani, baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya maji iliyomo katika majengo ya shule hiyo.

Shule hiyo ilikarabatiwa kuwapa hifadhi ya muda wanafunzi wa shule za sekondari Ihungo na Nyakato zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka jana.

Baada ya ukaguzi huo, Athumani alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chibunu Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika moja kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa shughuli hiyo.

Katika maelezo yake, Athuman alisema aligundua ukarabati uliofanywa ulikuwa chini ya kiwango na hauendani na thamani ya Sh milioni 119 zilizotolewa na Serikali.

“Kwanini wakurugenzi hampendi kufuatilia miradi iliyo katika maeneo yenu? Kama mngefuatilia mapema, mngegundua ubadhilifu uliofanyika hapa na kuchukua hatua mapema.

“Kwa hiyo, naagiza kuanzia leo Januari 3 (jana), mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba uwasimamishe watumishi wote waliohusika ambao ni Mhandisi Kitengo cha Ujenzi wa Manispaa ya Bukoba, Andondile Mwakitalu, Mhandisi Msaidizi, Costane Felix na fundi Charles Kafumu.

“Hawa lazima wasimamishwe ili kupisha uchunguzi utakaofanyika kwa ajili ya kulinganisha kazi iliyofanywa na kiasi cha fedha kilichotumika kama vinaendana.

“Tatizo jingine nililoligundua ni kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kutoka kwa watumishi wa manispaa. Hao nao uchunguzi dhidi yao utafanyika kwa uwazi na ukweli na hatutamwonea mtu.

“Sitaki kusikia shughuli hii inasimama eti kwa sababu ya hawa watu wamesimamishwa, fanya makabidhiano na wale watakaokuwapo.

“Kaimu mkurugenzi hakikisha mnakabidhiana kila kitu, hata msumari usibaki na uchague watu wengine wa kuendelea na kazi ya kusimamia mradi huu ili ukamilike kwa muda uliopangwa,”alisema.

Naye Mhandisi Mwakitalu aliyesimamishwa, alisema majengo hayo yalikuwa katika hali mbaya na kwamba ukarabati wake unahitaji fedha nyingi ili yarudi katika hali yake ya kawaida.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top