NA; BASHIR NKOROMO
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaridhishwa sana na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli kwa kuwa serikali hiyo imejikita ipaswavyo katika kutekeleza ilani ya Chama ikiwemo kuipeleka Tanzania katika nchi ya Uchumi wa Viwanda.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole, amesema, CCM imefikia hatua ya kutoa tamko rasmi la kuridhishwa kwake na utendaji kazi wa Serikali hiyo, baada ya Chama kufanya ziara ya uhakiki wa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo katika mkoa wa Pwani.
Hivi karibuni CCM ilipata fursa ya kushiriki katika ziara ya Rais Dk. John Magufuli katika mkoa huo wa Pwani, kwa kuwakilishwa na Polepole, ambapo katika ziara hiyo ya siku tatu, Rais alitembelea na kuzindua viwanda kadhaa ambavyo vinaonyesha kuwa vitachangia kwa kasi kuleta mahuisha matumaini ya lengo la Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa Viwanda.
"Katika kipindi cha miaka miwili cha Uongozi Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli, mkoa wa Pwani pekee, umeweza kuwa na viwanda vikubwa, vya kati na vidogo zaidi ya 370, hii ni hatua kubwa sana inayoonyesha kuwa Serikali hii imedhamiria kuifikisha Tanzania katika Uchumi wa Viwanda", alisema Polepole.
Polepole amesema, kufuatia uhakiki iliofanya CCM katika hivyo viwanda zaidi ya 370, viwanda 87 ni vikubwa ambavyo vina uwezo wa uzalishaji bidhaa hadi za kwenda nje ya nchi na kwenda katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba viwanda hivyo vilivyopo mkoa wa Pwani baadhi vimejengwa kwa ubia wa serikali na wadau na vingine wadau wenyewe.
Alisema, miongoni mwa viwanda vilivyoivutia CCM ni kile cha dawa za kuua viluwiluwi vya mbu ambacho ndicho pekee kilichopo Bara la Afrika na kwamba kiwanda hicho kimejengwa kwa ubia wa Serikali ya Tanzania ya Cuba. "Lakini cha kufurahisha zaidi ni kwamba Mheshimiwa Rais Dk.Magufuli ameshanunua lita 100,000 za dawa hiyo ambayo itasambazwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kupambana na malaria", alisema Polepole.
Polepole alisema, kiwanda kingine ni cha kutengeneza Nondo kilichopo Mlandizi Kibaha, ambacho alisema, kina uwezo wa kuzalisha tani 1000 za nondo kwa siku, na kina uwezo wa kutengeneza mataruma ya reli kwa kutumia malighafi za hapa nchini.
Kiwanda kingine alikitaja kuwa ni cha kuchakata matunda kilichopo Msoga, ambacho alisema, kina uwezo wa kuchakata tani 30 za matunda kwa siku, na kueleza kwamba uwepo wa kiwanda hiki utasaidia sana kuinua uchumi wa wakulima wa matunda katika mkoa wa Pwani, na kwa kutambua hivyo CCM imewaelekeza viongozi kuhakikisha maofisa ugani wanafika kwa wakulima kutoa elimu ya kilimo cha zao hilo, ili usije kutokea uhaba za matunda kiwanda kitakapoanza kuzalisha.
Polepole alisema, kwa kuzingatia kuwa umadhubuti wa viwanda unaendana pia na Kilimo, CCM imefurahi kuona kuwa imejengwa karakana na kuunga matrekta na kwamba hadi sasa inamalizia matrekta 140 ambayo alisema, yatauzwa kwa bei nafuu kwa kuwa yanaunganishwa hapa nchini.
Alisema, katika awamu ya pili Karakana hiyo ambayo imejengwa kwa ubia kati ya Tanzania na Uholanzi, mitambo itahamishiwa katika eneo la Tamco, Kibaha na badaa ya kuunganisha tu itakuwa ni kiwanda cha kutengenezea hapa nchini matrekta na pia kitakuwa kikiunganisha mabasi aina ya TATA.
UCHAGUZI NDANI YA CHAMA
Akizungumzia Uchaguzi ndani ya Chama, Polepole alisema, Chaguzi za Mashina zimeshakamilika nchini kote kwa asilimia 95, huku akiwataka Wanachama wa CCM wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za Jumuia na Kata huku akisisitiza kuwa fomu hizo zinatolewa bure.
"Wewe ukijisikia kuwa ni Mwanachama ambaye kwa dhati ya moyo wako unakerwa na shida za wananchi, unajiheshimu, ni mnyenyekevu lakini mkali dhidi ya maovu kachukue fomu kuombe ridhaa ya kugombea nafasi unayotaka", alisema Polepole.
Alisema, fomu katika ngazi za Jumuia na Kata zimeanza kutolewa tangu Juni 20, mwaka huu, na bdo zinaendelea kutolewa hadi mwezi ujao.
PONGEZI KWA JPM
Kadhalika, Polepole alisema CCM inaipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli kwa Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme katika mto Rufiji na kwamba hiyo ni hatua muhimu kwa kuwa inaendana na lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa viwanda kwa sababu umeme ndiyo kichocheo kikubwa cha viwanda.
Pia CCM imempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa Serikali yake kupeleka miswada Bungeni kwa minajili ya kurekebisha sheria kuhusiana na ulinzi wa madini na maliasili za nchi.
KUTOREJEA MASOMONI BAADA YA KUJIFUNGUA
Akizungumzia kuhusu kauli aliyotoa hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli kutoruhusu Wanafunzi kutorejea katika utaratibu wa kawaida wa masomo shuleni, Polepole alisema, CCM inampongeza Rais kwa kauli hiyo na inamuunga mkono kwa dhati kabisa.
"Mnajua baada ya Rais kutoa kauli hii, kuna baadhi ya watu wanajaribu kupotosha, ukweli ni kwamba Rais yupo sahihi na sisi CCM tunamuunga mkono. Mnajua utaratibu na ni kwamba mtoto anapopelekwa shuleni anaanza masomo katika mfumo rasmi, sasa anapopata ujauzito na kwenda kujifungua, haiwezekani tena kurejea masomoni katika mfumo huo. Lakini Siyo kwamba mfumo huo ndiyo wa mwisho, akipenda kuendendelea na masomo ipo mifumo mingine nje ya mfumo rasmi ambayo anaweza akasoma", alisema.
Matukio makuu Afrika 2024
4 hours ago
Post a Comment