Ofisi ya Bunge inapenda kuuarifu umma kuwa Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb), amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika.
Uchaguzi huo umefanyika katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliomalizika jana Mjini Abuja.
Kwa wadhifa huo, Mhe Ndugai ataongoza Maspika wenzake toka Mabunge na Mabaraza ya kutunga Sheria 63 yaliyoko katika nchi 18 za Jumuiya ya Madola kwenye Bara la Afrika.
Wadhifa huo ni wa miaka miwili kuanzia sasa hadi mwaka 2019 kutakapofanyika uchaguzi mwingine.
Nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Barani Afrika ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botwana, Cameroon ,Ghana, Kenya, Lesotho, Msumbiji, Mauritius, Malawi, Nigeria, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Swaziland, Tanzania, Uganda na Zambia.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mhe Ndugai amesema "Kwa hakika nawashukuru Maspika wenzangu kwa kunipa dhamana hii ya kuwa Mwenyekiti wao, ni heshima kwangu binafsi lakini zaidi Kwa Tanzania. Ni matumaini yangu kwamba Bunge letu litaendelea kung'ara kitaifa na kimataifa tukiwa Bunge moja lenye Upendo na mshikamano".
Huu ni wadhifa wa nne kwa Mhe. Ndugai katika masuala ya Bunge kwenye medani ya Kimataifa. Amewahi kuwa Mwakilishi wa Nchi za Afrika Mashariki katika Kamati ya Utendaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Duniani mwaka 2008-2011, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ya Umoja wa Mabunge ya Afrika, Pacific na Carribbean na Jumuiya ya Ulaya mwaka 2011-2014 na Rais wa Baraza la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC – PF)
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA
Ondoka na Mkwanja na Mechi za Kimataifa
35 minutes ago
Post a Comment