Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Vigogo wanne watupiwa mikononi mwa Takukuru

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi vigogo wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Mbozi na kuwakabidhi mikononi mwa kamanda wa mkoa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Damian Sutta.

Viongozi waliosimamishwa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Eliesai Ngowi, Bahati Chomoka kutoka Idara ya Uhasibu, Ofisa Ugavi, Remmy Haule na Mtunza Hazina, Noel Simon.

Wanatuhumiwa ukosefu wa maadili ya kazi za umma, kukithiri kwa vitendo vya kifisadi na rushwa vinavyoikumba wilaya ya Mbozi na kupelekea halmashauri hiyo kupata hati chafu miaka minne mfululizo.

Majaliwa alichukua hatua hiyo katika kikao cha watumishi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Vwawa.

Waziri Mkuu aliwaeleza watendaji hao kuwa anafahamu kila kitu kinachofanyika kwenye halmashauri hiyo na kuwataka watumishi waliosimamishwa kujieleza, lakini wakashindwa kutoa maelezo ya kutosha.

Majaliwa alieleza kuwa kwa zaidi ya miaka 10 kumekuwa na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma katika halmashauri hiyo, ikiwamo kufanya malipo ya fedha kwa kampuni hewa ya utengenezaji wa magari ya halmashauri kinyume na taratibu.

Alisema kuna kampuni hewa zaidi ya tatu ambazo zinatumika kulipa fedha ambazo viongozi hao wanapita kwa mlango wa nyuma na kuzichukua wakati wakijua kuwa ni fedha za umma.

Aidha, Majaliwa alisema mwenyekiti wa halmashauri, Erick Ambakisye kutokana na kukana kuhusika, amepewa angalizo kali.

"Haiwezekani wananchi wapate shida wakati serikali inaleta fedha ambazo hazifanyi kazi," alisema Majaliwa na kuagiza "kuanzia leo, mkurugenzi na watu wako nikitoka katika ukumbi huu, muhakikishe mnatoa ushirikiano kwa kamanda wa Takukuru kuonyesha mkataba na tini namba za kampuni."

Aliwakabidhi watumishi hao mikononi mwa Takukuru na kuwapiga marufuku kufanya kazi za umma mpaka uchunguzi wao utakapokamilika na ripoti hiyo kumfikia haraka kwa ajili ya maamuzi zaidi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameelezea kusikitishwa na kitendo cha halmashauri hiyo kongwe nchini kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato licha ya kuwa na vyanzo vingi.

Serikali iliagiza halmashauri zote nchini kukusanya si chini ya asilimia 80 ya bajeti, lakini Songwe imekusanya asilimia 72.

Majaliwa alimwagiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha anasimamia fedha za halmashauri na kwamba waliosalimika kutumbuliwa wajiandae kwani atarudi tena kuwashughulikia sambamba na viongozi wa halmashauri nyingine, ikiwamo Tunduma ambayo imekusanya asilimia 54 pekee ya mapato.

"Halmashauri ya Mbozi imekuwa shamba la bibi nafahamu hilo," alisema.

"Nitarudi tena kuwashughulikia watendaji wabadhirifu, (na) natoa rai kama yupo ambaye hawezi kuendana na kasi ya Rais (John) Maghufuli aachie ngazi mwenyewe."

Kufuatia maamuzi hayo ya Waziri Mkuu, watendaji wa ngazi ya chini na wananchi waliohudhuria kikao hicho walishangilia na kupiga mayowe, wakiashiria kuunga mkono maamuzi hayo.

Mpaka msafara wa Waziri Mkuu unaondoka ukumbini hapo, tayari watumishi hao walikuwa mikononi mwa Takukuru.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top