Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Waziri Mkuu akoleza moto sakata la vyuo vikuu 19 kufungiwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepigilia msumari sakata la vyuo vikuu 19 kuzuiwa udahili na kuvitaka kufanyia kazi kasoro zilizoainishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) badala ya kulumbana.

Juzi, TCU ilivifungia vyuo 19 kudahili wanafunzi pamoja na kuzuia kozi 75 katika vyuo 22 nchini kutokana na kasoro mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya siku tatu ya Vyuo Vikuu nchini, Majaliwa alivitaka vifuate utaratibu na si vinginevyo.

Waziri Mkuu pia alitoa wito kwa TCU na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), kuhakikisha kuwa programu zote zinazotolewa na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kupata ajira au kujiajiri na kuhimili ushindani kimataifa.

Aliwataka waweke mikakati ya kuinua viwango vya taaluma ili kuwa na tija kwa maendeleo ya nchi na dunia kwa ujumla, huku akizitaka taasisi za elimu ya juu kuangalia tena mitalaa yake ili iende sambamba na dunia ya kazi na ajenda za maendeleo ya Taifa.

“Waimarishe mfumo wa ithibati na ubora wa elimu na mafunzo ili kuhakikisha wanafunzi wanaohitimu shahada wanachangia maendeleo,” alisema Majaliwa.

Mbali ya Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa Simon Msanjila pia alivitaka vyuo vikuu vilivyoandikiwa barua na kupewa maelekezo ili kufanya marekebisho, kuyawasilisha TCU badala ya kutafuta njia ya mkato.

Aliwataka wenye vyuo kutatua changamoto zao na kuwaambia wasitarajie kwamba watatumia ofisi yoyote ya Serikali au kiongozi kuwasaidia.

Alisema wizara haitakivumilia chuo kikuu chochote kitakachotoa elimu yenye upungufu.

Profesa Msanjila alisema TCU itawachukulia hatua wanaoendelea kujitangaza licha ya kufungiwa kudahili, kwa sababu kufanya hivyo ni kuwadanganya wananchi.

Pia, alivitaka vyuo vikuu kufuata ada ya usajili iliyoelekezwa na Serikali ambayo haipaswi kuzidi Sh10,000.

Maoni ya wadau

Msimamo huo wa Serikali umeungwa mkono na baadhi ya wadau. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Profesa Joe Lugalla alisema hatua hiyo ni sahihi na inastahili kufanyiwa kazi.

Alisema waliliona hilo mapema ndiyo maana wapo makini katika udahili na kozi wanazotoa, ubora wa kozi hizo, na kuwa na walimu waliobobea katika taaluma mbalimbali.

Alisema wamejikita katika mambo mawili, afya na elimu, kwa sababu hakuna nchi itakayoendelea kama wananchi hawana afya na utaalamu wa kuelewa matatizo na kutafuta mbinu za kuyatatua.

Msemaji wa Chuo Kikuu cha Katoliki Mwenge cha Moshi, Athanas Sing’ambi alisema chuo hicho kimefungiwa kudahili kozi moja ya ‘Bachelor of Arts in Philosophy with Ethics’.

“Tumekubali kwa sababu kozi hiyo haikuwahi kuwa na wanafunzi,” alisema.

Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John ambaye hakuwa tayari jina lake kutajwa gazetini alilalamikia uhakiki huo kwa ujumla.

Alisema walipewa barua wiki mbili zilizopita na wamejibu baada ya wiki moja, lakini wanashangaa kabla hawajapata majibu, jina la chuo chao limo katika orodha ya waliozuiliwa kudahili.

“Sipingi maboresho, bali kama wanataka sekta binafsi iwe imara, tungekaa pamoja wakatupa maelezo tukashirikiana nao kutatua changamoto zilizojitokeza kuliko kutukomoa hasa katika kipindi hiki cha udahili,” alisema.

TCU wamezitaja sababu za kuvifungia vyuo hivyo kuwa ni pamoja na kutokuwa na walimu, vifaa na kutokidhi vigezo kitaaluma.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top