Na. Ahmad Mmow,Lindi.
WAKUU wa wilaya na mikoa nchini wametakiwa wasimamie halmashauri zilizopo kwenye maeneo yao ya utawala ili kuhakikisha zinashugulikia migogoro ya ardhi haraka.
Agizo hilo limetolewa na waziri wa nchi ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa maonesho ya 24 ya wakulima (Nane nane) kitaifa, katika viwanja vya Ngongo manispaa ya Lindi.
Simbachawene alisema wakuu wa mikoa na wilaya hawanabudi kuzisimamia halmashauri ili zishugulikie migogoro ya ardhi haraka na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji ardhi katika halmashauri zilizopo kwenye maeneo yao ya utawala. Ambapo pia amewataka wasimamie na kuhakikisha mipango ya matumizi bora ya ardhi inaandaliwa, ili kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Waziri huyo mwenye dhamana ya tawala za mikoa na serikali za Mitaa alisema wakuu wa wilaya na mikoa hawana budi kuzingatia maagizo na maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi yanayohusiana na masuala mbalimbali. Huku akiongeza kuwataka wasimamie na kuhakikisha zoezi la upigaji chapa mifugo linafanyika, hakuna mazao ghafi yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi , hakuna shuguli na kazi za kibinadamu zinazofanyika kwenye vyanzo vya maji na wasimamie na wahakikishe pia taasisi mbalimbali za biashara, ikiwamo TRA, TFDA na TBS zinaondoa vikwazo vya biashara kwa wananchi na wadau wengine.
Aliongeza kusema wawakilishi hao wa Rais katika maeneo yao ya utawala wawasimamie kikamilifu wakulima na wafugaji na kutoa elimu inayohusu usindikaji wa mazao yao ili waweze kuongeza thamani itayosababisha wauze kwa bei mzuri. Huku serikali ikitarajia bidhaa za aina hiyo zitaanza kuonekana, kuuzwa na kununuliwa katika supamaketi zilizopo hapa nchini.
"Natarajia nianze kuona viazi vya Gairo, mafuta ya alizeti yanayopangwa barabarani njia ya Singida, Dodoma hadi Morogoro, Nyanya zinazouzwa pale njiani eneo la mtandika njia ya Iringa na Dumila hadi Morogoro na maeneo mengine mbalimbali ya nchi hii yenye bidhaa za aina hiyo nataraji zionekane katika supamaketi zetu kwa namna ya kuwezesha usindikaji bora wa mazao hayo, "alisisitiza Simbachawene.
Mbali na hayo, Waziri huyo alitoa wito kwawananchi kutembelea viwanja vya maonesho ili waweze kujifunza mambo mbalimbali na kuwa tayari kuanza kutumia teknolojia na maarifa mapya watakayopta, ili kujiletea maendeleo na mapinduzi halisi ya kilimo. Lakini pia akiwaasa waoneshaji maonesho hayo wakidhi kiu na matarajio ya wananchi watakao tembelea, na wawape ushauri na maelekezo ya jinsi ya kuboresha shuguli zao za kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Loading...
Post a Comment