Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari na mwongozaji wa kipindi cha 360 cha Clouds TV, Hassan Ngoma katika mahojiano maalum kuhusu uzinduzi wa mradi wa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika Agosti 05, mwaka huu yaliyofanyika mapema Julai 31, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
*********
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo amewataka wananchi wanaoishi katika mikoa itakayopitiwa na miundombinu ya bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
Dkt. Pallangyo aliyasema hayo Jumatatu jijini Dar es Salaam kupitia kipindi maalum cha 360 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds wakati akielezea maandalizi ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa kufanyika Agosti 05, mwaka huu.
Alisema kuwa wananchi katika maeneo husika wanatakiwa kujiandaa kwa ajira wakati wa maandalizi na utekelezaji wa mradi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za vyakula, usafiri na ufundi.
“Fursa zitakazokuwepo ni nyingi mno, vijana waliomaliza Vyuo vya Ufundi wataweza kufanya kazi za uchomeleaji wa vyuma, madereva wenye leseni kupata kazi, wakina mama lishe kuuza vyakula, wakulima kuuza mazao kwa walaji watakaoongezeka kutokana na uwepo wa mradi huo, alisema Dkt. Pallangyo.
Akielezea manufaa ya mradi huo, Dkt. Pallangyo alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi za Uganda na Tanzania.Alisisitiza kuwa mradi utatoa takribani ajira 10,000 na kufungua fursa za biashara katika mikoa itakayopitiwa na mradi
“Mradi utapelekea kufunguka kwa Ukanda wa Biashara kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Rwanda, Burundi, Kongo, Sudan ambapo wanaweza kuunganishwa na miundombinu hiyo na kusafirisha mafuta kwa urahisi,” alisisitiza Dkt. Pallangyo.
Aliendelea kusema kuwa, kukamilika kwa mradi huo nchi za Tanzania na Uganda zitapata mapato na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wake.
Dkt. Pallangyo alieleza faida nyingine kuwa ni pamoja na gharama za mafuta kupungua kutokana na nchi za Afrika Mashariki kutumia mafuta yake yenyewe kwenye magari pamoja na ndege hivyo kuchochea kasi ya utalii katika nchi husika pamoja na ajira.
Awali akielezea mradi huo, Dkt. Pallangyo alisema kuwa mradi ulikuwa na ushindani mkubwa hata hivyo bado ilionekana Tanzania kuwa na vigezo vya bomba hilo kupita katika sehemu kubwa ya ardhi yake ambapo alieleza vigezo hivyo kuwa ni pamoja na hali ya tambarare katika ardhi ya Tanzania hivyo gharama za uwekezaji kuwa rahisi.
Aliongeza kuwa ardhi ya Tanzania ni rahisi pamoja na kuwepo kwa hifadhi ya barabara katika maeneo mengi hali inayopelekea gharama za fidia kuwa ndogo.
Dkt. Pallangyo alieleza vigezo vingine kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa na uzoefu mkubwa katika usimamizi wa bomba la Mafuta la TAZAMA na la Gesi linalotoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam.
“Pia bandari ya Tanga imeonekana inafaa kwa kuwa itawezesha mafuta kusafirishwa kwa mwaka mzima bila tatizo lolote,” alisema Dkt. Pallangyo.
Post a Comment