Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imekanusha taarifa iliyotolewa na uongozi wa CHADEMA kuhusu suala la ubinafsishaji na kuwa hakuna viwanda vipya vilivyojengwa katika awamu hii kwa vile hakuna mkopo wa kuanzisha viwanda.
Taarifa iliyotolewa Jijini Dar es Salam imesema kuwa viwanda vilivyokuwepo viliuzwa kwa bei rahisi kwa kuwa wawekezaji waliovichukua waliingia mikataba ya kuviendeleza na Serikali, hivyo vilichangia mapato ya serikali na kutoa ajira.
Aidha baadhi ya wawekezaji wa viwanda vilivyobinafsishwa waliviendeleza na mpaka sasa vimeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Baadhi ya viwanda hivyo ni Kiwanda cha Bia (TBL), Kiwanda cha Sigara (TCC), Viwanda vya Saruji vya Mbeya, Tanga na Twiga.
Hata hivyo viwanda vilivyokiuka mkataba vitarudishwa serikalini ili vitangazwe kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendeleza ili viendelee na uzalishaji ambao utatoa fursa ya ajira na kuingiza mapato serikalini.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa kwa kuwa viwanda hivyo vilijengwa kwa fedha za watanzania na kuuzwa kwa wawekezaji ili waviendeleze na wao wakavunja mikataba kwa makusudi nia ya kuvirejesha serikalini haina ubaya wowote.
Serikali imeendelea kujenga viwanda kutokana na kupata mikopo kutoka katika taasisi za kifedha za ndani.Viwanda hivyo ni Pipeline industries, Masasi Food Industries na CATA mining Ltd.
Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya viwanda 224 vilisajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), 41 kupitia Mamlaka ya maeneo maalum ya uwekezaji (EPZA), 128 kupitia BRELA na 2,143 kupitia shirika la viwanda vidogo(SIDO ).
Aidha wizara imetoa tahadhari kwa wawekezaji waliobinafsishiwa viwanda na hawajaviendeleza kuharakisha kuvifufua kwa mujibu wa mikataba yao kwani zoezi la kuvirejesha serikalini limeanza kwa kasi.
Watanzania wametakiwa kuendelea kutumia fursa zilizopo za kujenga viwanda ili kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa kati.
Source: Mpekuzi
Loading...
Post a Comment