Mwanamuzi
wa kizazi kipya nchini Abdul Nassib almaarufu kama Daimond Platnumz amekuwa
kwenye vichwa vya habari siku za hivi karibuni kufuatia kutuhumiwa kuzaa na
Mwanamitindo Hamisa Mobeto ambapo yeye Hamisa alikiri kuzaa nae lakini Daimond
Platinum alikuwa akikataa kataa mpaka leo hii Jumanne Septemba 19, 2017 Daimond
Platinum akiri kwa mara ya kwanza kuzaa na Hamisa Mobeto.
Daimond Platnum ameanika uhusiano wake
na Hamisa wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Leo tena cha Cloudsfm. Daimond Platnumz akiri Mtoto ni wake na alianza kuihudumia mimba
toka siku ya kwanza. Kila siku Hamisa Mobeto alikuwa anaenda kushinda Madale; Diamond
Platinumz amekiri kumnunulia gari aina ya Rav 4 Hamisa wakati akiwa mjamzito
kwa ajili ya kumpeleka kliniki; Diamomd humpa Hamisa Tsh. Laki 5 kila wiki ya
matumizi; Diamond Platinumz alimpa Tsh. Milioni 7 Hamisa kwa ajili ya kununua
vitu vya Mtoto na samani za ndani; Siku Diamond Platnum anarudi kutoka London
alienda kulala na Mwanaye na kushinda nae.
Daimond Platnum amekuja kukiri dakika ya mwisho
mara baada ya kuona Hamisa anaanza kuvujisha picha zao wakiwa faragha na kuona
itamchafulia.
Kisa hiki cha Daimond Platnumz nakifananisha na
kisa cha Wanasiasa wetu hapa nchini hususani wale wa vyama vya upinzani
wasiopenda kuongea ukweli wa mambo kwa wakati na kungojea tukio lipite ndio
kuja kukiri ukweli. Hii tabia ya kubadilika badilika haina tofauti na tabia au
hali ya unafki.
Tuweke kumbukumbu zetu sawa. Mwalimu Julius Nyerere
wakati akiwa madarakani alimwagiwa lawama na tuhuma lukuki kwani wapo waliosema
Mwalimu haambiliki na wengine wakadai anaendesha nchi kwa “remote” akiwa
Butiama (kijijini kwao). Lakini mara baada ya kung’atuka kwa hiari Urais ndipo
sifa za kinafki zilianza kummiminikia huku tukianza kumuita “Baba wa Taifa”. Mara baada umauti kumkuta ndipo unafki ulizidi
kwake na leo hii kila kitu kibaya kinachotokea tunasema laiti Mwalimu Nyerere
angekuwepo haya yote yasingetokea. Lakini angali hai ama madarakani
hatukuyatambua haya zaidi ya kuuendekekeza unafki.
Ama Alhaji Hassan Mwinyi wakati akiwa Rais wa awamu ya
pili walimwita mbinafsi, muuzaji nchi kutokana na ubinafsishaji lakini leo hii
ni mstaafu wanaanza kummwagia sifa teletele na hata kumwita “Mzee
wetu” huku wakijivunia kuchota hekima na busara kutoka kwake lakini angali
madarakani hatukuliona hilo. Huu ni unafki mtupu.
Pia Mzee Benjamini Mkapa alidhihakiwa kweli
kweli wakati wa uongozi wake hadi kufikia hatua ya kumwita ‘ukapa’ badala ya
Mkapa kutoka katika neno la ‘ukata’. Lakini leo hii kila anapokatiza ni
shangwe, makofi, vifijo, na vigelegele na tukisema afadhali ya Mkapa kuliko
wote na wengineo tumewaona wakimpa hata tuzo ya heshima. Jamani! Kama huu
si unafki, basi tuuiteje?
Hata Dk. Jakaya Kikwete (JK) alipokuwa madarakani
walimuita majina mengi ya hovyo hovyo. Wapo waliomuita “Mzee wa kutabasamu”,
Serikali yake ni dhaifa na legelege! Lakini hekima na busara kubwa aliyojaaliwa
Dk. Kikwete hakuweza kuwajibu lolote waliokuwa wakimkejeli na badala yake
aliwaambia mtanikumbuka.
Kikwete alisema: “Mtaumbuka baada ya 2015”. Dk. Kikwete
aliwaambia wanaombeza sasa wataona aibu baada ya kumaliza kipindi chake. Naam!
Ni kweli Watu waliokuwa wakimbeza wameanza kuumbuka na kunza kupayuka hadharani
kuwa wana mkumbuka.
Kama
kweli maisha yalikuwa mazuri kwanini walikuwa wakimkashifu mtu (JK) ambaye amewanyooshea
Watanzania maisha yao? Kulikuwa kuna sababu gani kwa Wapinzani kumfedhehesha
majukwaani kwamba Serikali yake ilikuwa dhaifu na maisha yalikuwa magumu? Leo
hii wanamponda Rais Magufuli, kwanini tusiamini kwamba akitoka madarakani nae
wataanza kumsifia?
Rais
Magufuli anafanya mambo mengi ya msingi kwa Taifa letu lakini Watu kwa maslahi
yao binafsi wanaamua kupindisha ukweli wa mambo tofauti na uhalisia waujuavyo
moyoni mwao. Hakuna asiyejua namna ambavyo Rais Magufuli anavyojitahidi
kutekeleza ilani ya uchaguzi.
Tangu Rais
Magufuli aingie madarakani tumeshuhudia Elimu Bure ikitolewa kuanzia ngazi ya
shule ya msingi mpaka Sekondari, Mikopo ya elimu ya juu ikiongezwa na kutolewa
kwa wingi, Wanafunzi wa vyuo vikuu wakijengewa hostel za kuishi, madawati
yakisambazwa mashuleni, maabara na maktaba zikijengwa mashuleni.
Ni katika
utawala wa awamu ya 5 ya Serikali ya Rais Magufuli tumeshuhudia vitanda, madawa
na vifaa tiba vikipatikana kwa wingi mahospitalini, huduma bure ya matibabu kwa
Wazee na utolewaji wa Bima za Afya ukifanyika, Hospitali zetu hapa nchini
zikitoa huduma za kibingwa za upasuaji wa figo, moyo na magonjwa mengineyo hapa
nchini, Serikali ikiboresha huduma za Mama Mjamzito na Watoto hapa nchini, Serikali
ikiboresha miundombinu ya hospitali na vituo vya afya nchini kwa kuhakikisha
huduma za kiafya zinapatikana jirani na wanapoishi na ziwe za uhakika.
Rais
Magufuli amehakikisha Taifa letu linakuwa kiuchumi na hatimaye kufikia uchumi
wa kati kwa kufufua mashirika ya umma yaliyokuwa yamesinzia kwa mfano kununua
ndege mpya 4, kununua hisa zote za kampuni ya simu nchini ya TTCL na hivyo
kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 hali iliyopelekea kampuni kuanza
kufufuka; kufufua kilimo kwa kuondoa kodi kwenye kilimo; Kuhakikisha anapambana
na madaw ya kulevya nchini; Kuhakikisha rasilimali zetu zinamnufaisha
Mtanzania, mfano kwenye sekta ya madini; Kujenga miundombinu ya Barabara,
vivuko, madaraja, boti, viwanja vya ndege, ujenzi wa reli ya kisasa ya hadhi ya
standard gauge, kujenga barabara za juu (flyovers); Kutengeneza fursa nyingi za
ajira kwa kuwatoa wasio na ajira halali na kuajiri wanaostahili kulingana na
sifa zao.
Rais
Magufuli ameendelea kuhakikisha anapunguza anasa Serikali kwa kuongeza pesa
zaidi za kwenye miradi ya kimaendeleo; Kupunguza kiwango cha rushwa nchini; Kuboresha
kiwango cha utendaji na uwajibikaji kwa Watumishi wa umma; Kuwaondoa kazini
mara moja wale wote wanaoleta mzaha kazini.Hayo ni kwa uchache sana wa mema
yanayofanywa na Serikali ya Rais Magufuli.
Kiukweli
Serikali ya awamu ya 5 ya Rais Magufuli inachapa kazi sana lakini ajabu yake
mara kwa mara asilimia kubwa ya Wapinzani wameshindwa kukubali utendaji wa
Serikali ya Rais Magufuli unaofanywa kwa sasa lakini akishatoka madarakani
utaona watakavyomsifia, Matukio ya kihistoria yanaonyesha hivyo.
Nampongeza
Mwanamuziki Daimond Platnum kwa kuonyesha ukomavu na ushujaa wa kukiri
hadharani juu ya Mtoto kuwa amezaa na Hamisa Mobeto kuwa ni wake na hakuwa na
sababu ya ziada kuendelea kusema uongo ili kupindisha ukweli. Ni wakati hata
kwa vyama vya upinzani, Wanaharakati nao pia kuiga mfano wa Mwanamuziki Daimond
Platnumz kukubali kusema ukweli mapema na kwa wakati, kuwa Mpinzani haina maana
kupinga kila kitu. Uzalendo huanza kwa kusema ukweli, tuwe wazalendo.
Na Emmanuel J. Shilatu
Post a Comment