Loading...
Wanakijiji washinda kesi ya kimataifa ya madini
*Wanakijiji Zambia washinda kesi ya awali dhidi ya kampuni madini ya kimataifa*
LONDON, UINGEREZA
TAKRIBAN wanakijiji 2,000 nchini Zambia wameshinda kesi ya kudai HAKI ya kuishitaki kampuni ya kimataifa ya Vedanta Resources inayoendesha shughuli za uchimbaji madini ya kopa kiasi cha kuwachafulia mazingira kijijini kwao.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya London, Uingereza, na uamuzi huo sasa unatajwa kutoa mwanya kwa kampuni nyingine za kimataifa kuweza kushitakiwa jijini London kuhusu shughuli zao nje ya nchi.
Oktoba 13 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa ya Uingereza ilitupilia mbali shauri la kampuni hiyo ya uchimbaji madini kuwazuia Wazambia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kashfa ya uchafuzi wa mazingira kwa wanavijiji hao, uchafuzi unaosabaishwa na shughuli zao.
Hata hivyo, kampuni ya Vedanta imedai kwamba itachukua uamuzi wa kukata rufaa kwenye Mahakama ya Juu (Supreme Court), mahakama ambayo ndio yenye uwezo wa mwisho kwa mujibu wa mfumo wa kimahakama wa Uingereza.
Majaji waandamizi watatu wa Mahakama Kuu walitupilia mbali shauri hilo la Kampuni ya Vedanta pamoja na kampuni yake tanzu ya uchimbaji madini inayoitwa Konkola Copper Mines (KCM).
Wanakijiji hao wamekuwa wakilalamika kwa kudai kuwa ardhi yao pamoja na maisha yao yameathiriwa mno na uchafuzi wa maji unatokana na shughuli za kampuni ya uchimbaji madini ya Nchanga Copper Mine, inayomilikiwa na kampuni ya Vedanta kupitia kampuni yao tanzu ya KCM.
Kampuni moja ya uwakili ya Uingereza, inayoitwa Leigh Day ndio iliyosimamia haki ya wanakijiji hao, shughuli ambayo ilifanywa katika makubaliano ya msaada - bila malipo yoyote, kampuni hiyo ya uwakili ndio chachu ya ushindi wa wanakijiji hao.
Raphael Karima, mmoja wa viongozi wa wanakijiji hao anasema, wenzake wanataraji mwendelezo wa ushindi dhidi ya kampuni hiyo kupitia mfumo wa kisheria.
Naye Martyn Day, mmoja wa washirika wa kampuni ya uwakili ya Leigh Day, anasema hukumu hiyo ni hatua muhimu katika kufanikisha juhudi za wanavijiji hao kudai haki yao.
Kampuni ya uwakili ya Leigh Day, tofauti na mgogoro huo wa wanavijiji wa Zambia ndiyo inayowasaidia kisheria wakazi ya Delta ya Niger katika kesi dhidi ya kampuni ya Uholanzi ya Shell katika mgogoro wa uchimbaji mafuta huko Nigeria, kesi ambayo itasikilizwa tena mwezi Novemba mwaka huu.
*Habari hii imetafsiriwa kutoka Shirika la Habari la Reuters*
Post a Comment