Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Hati za kumiliki Ardhi kutolewa ndani ya siku 30 tu

Serikali imeanza kutoa Hati za kumiliki ardhi ndani ya Kipindi cha Siku 30 tangu kupokelewa kwa maombi tofauti na awali ambapo mchakato wa kupata hati hizo ulichukua zaidi ya siku 90 ikiwa ni matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi hapa nchini.

Akizungumza katika kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania  (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO), Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa kila kipande cha Ardhi kinapimwa na kumilikishwa.

“Tumejipanga vizuri na sasa taarifa zote za Ardhi zitakuwa katika mfumo wa kielektroniki  utakaounganisha taarifa za nchi nzima hivyo tutaweza kudhibiti vitendo vyote vilivyokuwa vikifanyika awali kinyume na utaratibu na kuchochea kuongezeka kwa migogoro ya Ardhi hapa nchini,” alisisitiza Lukuvi

Ameendelea kwa kusema, hatua zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kutenga muda wa kuwasikiliza wananchi na kuzipatia ufumbuzi chanagamoto zinazowakabili ikiwemo kudhulumiwa viwanja ambapo Serikali imekuwa ikirudisha umiliki kwa wananchi husika pale inapojiridhisha kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo husika.

Aliongeza kuwa, mapato ya Serikali yemeongezeka kutoka milioni 46 hadi Bilioni 100 kwa mwaka ikiwa ni kodi ya Ardhi. Aidha, kuongezeka kwa mapato hayo kumetokana na usimamizi madhubuti wa Serikali katika sekta ya ardhi hapa nchini ili kuwapa wananchi wote fursa yakutumia ardhi na kujiletea maendeleo.

Vile vile amesema, hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuanzisha ofisi za Kanda zitakazokuwa zikitekeleza majukumu yanayotekelezwa na wizara ikiwemo kutoa hati ili kusogeza huduma kwa wananchi hasa wanyonge waliopo Vijjini ambao mara nyingi hushindwa kusafiri hadi makao makuu ya Wizara kufuata huduma hizo.

Pia Lukuvi alibainisha kuwa Serikali imenunua vifaa vya upimaji ardhi vitakavyotumika katika Ofisi za Kanda ili kuwawezesha watumishi wake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hali itakayosaidia sekta hiyo kutoa mchango mkubwa katika kujenga uchumi.

“Hati za Kimila elfu 46,000 zimeshatolewa kwa wananchi ili kuwawezesha kuwa na milki salama ambazo zitachochea maendeleo katika  maeneo yao kwani zinaongeza thamani ya ardhi ya eneo husika, vile vile maeneo  ya makazi zaidi ya  200,000 yametambuliwa na kurasimishwa,” alisisitiza Lukuvi

Aidha Mhe. Lukuvi amewaasa wamiliki wa mashamba makubwa kuyaendeleza vinginevyo Serikali itayatwaa na kuyamilikisha kwa wananchi ili wayatumie kwa shughuli za uzalishaji ambapo kwa sasa mashamba makubwa zaidi ya 150 yamefutiwa umiliki na kurudishwa kwa wananchi.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni moja ya Sekta muhimu katika kujenga uchumi wa Viwanda na imekuwa ikichukua hatua mahususi katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya Ardhi. Hatua hizo zinajumuisha ujenzi wa Kanzi Data ya taarifa za ardhi kwa nchi nzima na pia kuunganisha mifumo yake na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika kujenga uchumi wa viwanda.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top