Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

WAZIRI KAIRUKI AKUTANA NA SHIRIKISHO LA MADINI LA NCHINI INDIA


Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry) ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Uongezaji Thamani Madini ya Mawe yenye thamani ya Granite na Mable.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 18 Julai, jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki ameueleza ujumbe huo kuhusu adhma ya Tanzania kukakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa vinu vya kuyeyusha madini ya metali, usonara pamoja na ukataji na ung’arishaji madini ya vito hususan madini ya Tanzanite ambayo kwa kiasi kikubwa yamekua yakisafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi.

“ Sheria yetu ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017, imekataza usafirishaji wa Makinikia pamoja na madini ghafi nje, ndiyo maana tunakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini ndani ya nchi,” amesema Waziri Kairuki.

Pia, Waziri Kairuki amewashauri wawekezaji hao kukutana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuona namna bora ya kushirikiana katika miradi mbalimbali ikiwemo ya mawe yenye thamani, bati na madini mengine.

Vilevile, Waziri Kairuki amelitaka shirikisho hilo kuona namna ambavyo linaweza kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini nchini hususan katika masuala ya masoko na mitaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini ya Granite na Sekta ya Mawe la nchini India, Keshava Murthy, amemweleza Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo liko tayari kuwekeza kwenye madini ya granite pamoja na marble kwa kuanza na makontena kati ya 20-50 kwa mwezi.

Pia, Murthy ameongeza kuwa, Shirikisho hilo lina wanachama zaidi ya 1200 ambao wanajihusisha na shughuli za uongezaji thamani madini ya granite nchini humo.

Kuhusu ushirikiano na STAMICO, Murthy amemwahidi Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo litakutana na shirika hilo kwa lengo la kubadilishana ujuzi ikiwemo kuangalia namna bora ya kushirikiana katika sekta husika.

Aidha, amemweleza Waziri Kairuki kuhusu maonesho ya  mawe yenye thamani yanayojulikana kama STONA FARE ambayo huandaliwa na shirikisho hilo  na kuongeza kuwa, ni miongoni mwa maonesho makubwa duniani.

Mbali na kukutana na Waziri Kairuki, wawekezaji hao wanatarajia kuendelea na ziara jijiji Dodoma ambapo wanatarajia kukutana na na Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania, kutembelea Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye uchimbaji wa Granite jijini Dodoma.

Kabla ya kuja nchini, wawekezaji hao walitembelea nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji kwenye madini hayo.

Kikao hicho pia, kimehudhuriwa na Mwakilishi kutoka Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TIC), Wataalam kutoka Wizara ya Madini wakiongozwa na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki Mhandisi Ally Maganga aliyemuwakilisha Kamishna wa Madini.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top