Tume ya Warioba kutafuna bilioni 40/-
Kwa mwaka kila mjumbe kuvuna
zaidi ya milioni 300/-
Wasio wajumbe yaani watumishi kutumia bilioni 4.3/-
Sh bilioni 2.0 kulipia nyumba wafanyakazi wa Sekretariati
Wasio wajumbe yaani watumishi kutumia bilioni 4.3/-
Sh bilioni 2.0 kulipia nyumba wafanyakazi wa Sekretariati
Jaji Joseph Warioba
Serikali imefanya kufuru ya kutenga Sh. bilioni 40/- kwa ajili ya wajumbe 34 wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba. Kwa mujibu wa kasma ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoko kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/13.
Iliyopewa jina la Vote Number 8 (Fungu namba 8), wajumbe 34 wa tume hiyo wametengewa posho ya Sh. bilioni 10 watakayolipwa kwa kipindi cha mwaka mmoja jambo ambalo baadhi ya wabunge wamesema hawaridhiki na kuhoji serikali inatafuta kitu gani kwa tume hiyo.
Wajumbe wa kawaida wa tume hiyo kwa mujibu wa
mchanganuo wa bajeti, watalipwa posho ya Sh. karibu 450,000 kwa siku lakini
Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti wa Tume fungu lao ni kubwa zaidi ambalo
limeongezewa viburudisho na takrima.
Kwa mujibu wa taarifa za uchambuzi wa posho hizo,
kila mjumbe kuanzia mwaka wa fedha wa Julai 2012 hadi Julai 2013, atakuwa
amejikusanyia zaidi ya Sh milioni 294 jambo ambalo baadhi ya wabunge waliohojiwa
na NIPASHE Jumapili walisema ni maajabu ya Firauni.
Pamoja na kuhakikishiwa kuwa na ukwasi mkubwa, pia
wametengewa Sh. milioni 10 kwa ajili ya matibabu kwa wale ambao wameelezwa kuwa
hawapo kwenye utaratibu wa kugharamiwa tiba na serikali.
Dau kubwa ambalo lipo kwenye bajeti hiyo kwa
mujibu wa wabunge hao ambao wameomba majina yao yasitajwe, ni kutengwa Sh.
milioni 250 zinazodaiwa zitatumika kwa ajili ya usafi na ulinzi wa ofisi za Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao 34 kutoka Bara na Visiwani wametengewa
Sh milioni 10 kugharamia mazishi na kuwasafirisha wajumbe wa tume hiyo
watakaofariki dunia wakati wakiwa kwenye mchakato wa kukusanya maoni.
Sambamba na hilo, tume hiyo imetengewa zaidi ya
Sh. bilioni 10 kununua magari 56 ambayo sita kati yake ni Land cruiser heavy
duty zenye mikonga zitakazofungwa vipaza sauti ili kukusanya watu watoe maoni
yao na mengine 50 yatakuwa ni mashingingi ya kisasa maarufu kama V8. Kwa sasa
tume hiyo inadaiwa kuazimwa magari kutoka Wizara ya Sheria na Katiba.
Baadhi ya wabunge waliliambia gazeti hili kuwa
bajeti na idadi ya magari imepunguzwa badala ya kutumia Sh. bilioni 10
zitatumika Shilingi bilioni sita na kwamba yatakayonunuliwa ni magari 26 badala
ya 56 lakini idadi ya Land cruiser heavy duty zitakazofungwa vipaza sauti
haijabadilika.
Ofisi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia
inatarajiwa kutumia Sh milioni 256 kugharamia umeme na maji ambapo kila huduma
imepangiwa kugharimu karibu Sh milioni 128, yaani umeme Sh. 127,992,000
kadhalika maji nayo yamepangiwa kugharimu kiasi hicho na kuwafanya wabunge
wachambuzi kuhoji sababu za gharama za umeme na maji kufanana.
Tume hiyo imetengewa posho ya takrima iliyoitwa
hospitality services ya jumla ya Sh. milioni 300 huku simu za TTCL pamoja na
gharama za nukushi (fax) zikifikia karibu Sh. milioni 127 wakati zile za mkononi
zitawagharimu walipa kodi zaidi ya Sh. milioni 91.2.
WAFANYAKAZI WA SEKRETARIATI YA
TUME
Kundi hili sio la wajumbe bali hawa ni watumishi
wa ofisini watawala, wahasibu, makatibu muhtasi, wafagizi, wataalamu wa
kompyuta, madereva na wengine nao wametengewa mafungu kadhaa ikiwemo posho ya
kujikimu wakisafiri nayo ni Sh bilioni 4.3.
Kingine ambacho wabunge waliochambua Vote No 8 ama
fungu hilo walisema kilichowashangaza ni kutenga Sh bilioni 2.0 kwa ajili ya
kulipia nyumba za wafanyakazi wa Sekretariati ya Tume na kuhoji hivi wafanyakazi
hao hawana nyumba jambo lililoelezewa na wawakilishi hao wa wananchi kuwa ni
ulaji ambao wanasubiri kuuhoji wakati serikali ikiwasilisha bajeti hiyo.
Pia wafanyakazi hao ambao watalipwa posho ya Sh.
50,000 kwa siku wametengewa Sh. milioni 300 kwa ajili ya kununulia vifaa vya
chai ambavyo havikuelezwa ni vitu gani pamoja na vitafunwa. Tume ya Mabadiliko
ya Katiba inaongozwa na Jaji Joseph Warioba ambaye ni Mwenyekiti wakati Makamu
Mwenyekiti ni Jaji Augustine Ramadhani.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
Post a Comment