|
VIGOGO
wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kuhusika katika sakata la
uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia kupitisha makadirio ya
matumizi ya wizara hiyo ya 2011/2012 watafikishwa mahakamani, Mwananchi
limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa
umebaini kwamba hivi sasa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) anafanya ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) ambao unaweza
kubaini kuwapo kwa makosa ya kijinai katika utaratibu huo.
Ukaguzi
wa sasa wa CAG ni sehemu ya mchakato wa kukamilisha taarifa ya Serikali
kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya Novemba 11, mwaka jana
kuhusu uchangishaji wa fedha hizo ambao uliratibiwa na aliyekuwa Katibu
Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.
Baada ya kusomwa kwa
taarifa hiyo, Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe iliahidi kuyafanyia kazi na
kuwasilisha majibu Bungeni.
“Kwa sababu ya ukubwa na uzito wa
taarifa hii, ni vigumu kuitolea majibu yote hapahapa, ninachoweza
kufanya ni kuipokea pia tutakapokuja katika Mkutano wa Sita, tunategemea
kuleta majibu ya hoja zilizomo kwenye taarifa hii,” alisema Chakawe
ambaye sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria. Kauli ya CAG
CAG,
Ludovick Uttouh akizungumza na Mwananchi alikiri ofisi yake kufanya
ukaguzi huo ambao alisema unajulikana kama ‘ukaguzi wa utambuzi’ lakini
akasema kazi hiyo ilikuwa bado haijakamilika. Hata hivyo, alisema
hafahamu ni lini ukaguzi huo utakamilika.
“Niseme kwamba katika
ukaguzi wa aina hii tunakwenda ndani zaidi na mara nyingi huwa unalenga
kubaini iwapo kuna jinai katika hesabu zinazohusika na ukaguzi,” alisema
Uttouh.
Mtaalamu mwingine wa ukaguzi wa hesabu anasema ukaguzi wa
aina hiyo hufanywa ili kubaini kuwapo kwa makosa ya kimahesabu ambayo
yatawezesha kubaini makosa ya jinai na hatimaye wahusika kufikishwa
mahakamani.
“Huu ni utaratibu au niseme ukaguzi wa hesabu ambao
lengo lake huwa ni kutafuta ushahidi wa kuwapo kwa makosa ya jinai kama
rushwa au matumizi mabaya ya fedha,” alisema mmoja wa wataalamu wa fedha
katika Wizara ya Fedha na Uchumi (jina tunalo).
Moja ya
mapendekezo ya Kamati teule iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini,
Ramo Makani ambayo baadaye yaliazimiwa na Bunge ni kuwachukulia hatua
za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, watumishi wote wa Wizara ya Nishati
na Madini waliotajwa kwenye taarifa hiyo.
Katika taarifa yake,
Kamati Teule ilisema utaratibu wa uchangishaji wa fedha Sh418.081
milioni uliofanyika katika wizara hiyo haukuwa na uhalali kwa mujibu wa
Katiba, Sheria na Kanuni za Fedha za Umma.
Kadhalika, Bunge
liliazimia kwamba ufanyike ukaguzi wa kiuchunguzi (forensic audit) wa
matumizi ya Sh214 milioni ambazo kati ya hizo, Sh126 milioni, Kamati
Teule ilikataa maelezo ya matumizi yake na Sh88 milioni ni zile
zinazotajwa kwamba zilitumika katika kugharimia semina kwa wabunge.
Azimio
jingine ni lile lililoitaka Serikali iviagize vyombo vya dola kufanya
uchunguzi juu ya tuhuma za kughushi na ubadhirifu zilizoelezwa ili hatua
za kisheria ziweze kuchukuliwa kama ilivyoelekezwa.
Kwa maana
hiyo ikiwa uchunguzi na CAG utafanyika na kubaini jinai, huenda wahusika
waliotajwa katika ripoti hiyo wakafikishwa mahakamani kwa makosa
yatakayobainishwa.
Serikali katika hatua za mwisho Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi
alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, Serikali iko katika hatua za
mwisho za kukamilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge.
“Tuko
katika hatua nzuri sana na ikiwa Spika atatupa nafasi katika Bunge
hili, Serikali iko tayari kuwasilisha majibu ya jinsi tulivyofanyia kazi
maazimio yale ya Bunge,” alisema Lukuvi.
Waziri huyo alisema
Serikali tayari ilikuwa imekamilisha kazi yake lakini ilikuwa ikisubiri
pande mbili nyingine muhimu ambazo zilikuwa zikikamilisha kazi yake ili
taarifa kamili iweze kuandaliwa na kuwasilishwa kwa Spika.
Hata
hivyo, Lukuvi hakuwa tayari kutaja pande hizo mbili muhimu zaidi ya
kusema tu kwamba: “Wewe fahamu kwamba tumeyafanyia kazi maazimio ya
Bunge na majibu yapo tayari ikiwa tutapewa nafasi hata kama katika Bunge
hili.”
Uchunguzi zaidi umebaini kwamba pande hizo mbili ni Ofisi
ya CAG na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ilikuwa
ikiyafanyia kazi masuala ya kisheria katika maazimio hayo ya Bunge.
Majibu
ya Serikali kuhusu maazimio ya Bunge yalipaswa kuwasilishwa katika
Mkutano wa Sita wa uliofanyika Februari, mwaka huu lakini haikuwezekana
kutokana na Serikali kutokuwa tayari.
Katika mkutano uliofuata wa
saba ambao ulifanyika Aprili, mwaka huu, Serikali iliwasilisha taarifa
hiyo lakini Spika Anne Makinda aliirejesha kutokana na kubaini kuwa
majibu yake hayakuwa yakikidhi matakwa ya maazimio ya Bunge.
Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Bunge lilikuwa halijapokea taarifa
au kusudio lolote la Serikali kuwasilisha majibu ya maazimio hayo katika
kikao cha Bunge la Bajeti... “Kwa sasa sidhani kama kuna taarifa hiyo,
ila wakiwa tayari nadhani watatuarifu na taratibu zitafuata.”
Maazimio ya Bunge Mbali
na kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa ziada ili kubaini iwapo kulikuwa
na jinai katika sakata hilo pia kutaka Jairo achukuliwe hatua kwa
kuvunja sheria, kanuni na taratibu za fedha za umma na kuruhusu matumizi
mabaya ya fedha za umma, pia kulikuwa na maazimio mengine kadhaa
likiwamo la Serikali kutumia mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuainisha
taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa na mihimili mitatu ya Dola nchini
katika kutekeleza majukumu yao.
Kamati hiyo iliutaja muundo wa
Bunge kuhusu utaratibu wa sasa wa Serikali kuwa ndani ya Bunge, mawanda
(scope) ya mamlaka ya Bunge kuisimamia na kuishauri Serikali na
mawasiliano baina ya mhimili mmoja na mwingine hasa katika mambo
yanayogusa haki na madaraka ya mhimili zaidi ya mmoja.
Bunge
lilitaja eneo jingine kuwa ni mipaka na ushirikishwaji wa mamlaka
mbalimbali ndani ya mhimili mmoja wa Dola katika utekelezaji wa majukumu
ya mihimili hiyo kusimamiana, kurekebishana na kukosoana bila ya
kuathiri masharti ya sheria na katiba (checks and balances).
Maazimio
mengine ni sheria, kanuni na taratibu zilizopo kufanyiwa marekebisho
ili kutoa nafasi kwa makatibu wakuu kuwashirikisha mawaziri katika
uamuzi wa kiutendaji hasa katika matumizi ya fedha.
“Hatua hii
itawapa fursa mawaziri kutekeleza vizuri zaidi majukumu yao wakiwa
wasimamizi wakuu wa uamuzi wa shughuli za Serikali Wizarani,” inasomeka
sehemu ya maazimio hayo ya Bunge.
Pia Bunge liliazimia Serikali
ifanye mapitio ya Sheria ya Utumishi wa Umma ili kuweka utaratibu
utakaowezesha mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wanaoteuliwa na Rais
inaposhughulikia masuala ya nidhamu, ifanye hivyo kwa kuyaarifu mamlaka
hayo ya uteuzi na Waziri Mkuu ambaye ni msimamizi mkuu wa kazi za
Serikali.
Liliazimia kuwa Serikali iunde chombo maalumu cha
kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaoteuliwa na
Rais na kwamba itoe mwongozo kuhusu malipo posho ya takrima, ili
kuainisha viwango vya posho hizo.
Azimio jingine ni lile
lililoitaka Serikali itoe mwongozo kuhusu idadi ya maofisa wanaopaswa
kwenda Dodoma kwa ajili ya mikutano ya Bunge na katika mwongozo matumizi
ya teknolojia ya habari na mawasiliano, yasisitizwe ili kupunguza idadi
ya maofisa hao.
Chanzo: Mwananchi
|
on Thursday, July 19, 2012
Post a Comment