NYASI za
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo zinatarajiwa kuhimili patashika tena ile ya
nguo kuchanika, wakati washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita, Azam
FC watakapomenyana na washindi wa tatu, Yanga SC katika fainali ya Klabu Bingwa
ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Hii inakuwa
mara ya pili mfululizo, kwa fainali ya michuano hiyo kukutanisha timu za Dar es
Salaam pekee, mwaka jana mabingwa watetezi, Yanga wakitwaa taji hilo kwa
kuwafunga watani wao wa jadi, Simba SC 1-0 bao pekee la mshambuliaji ambaye
amekwishatupiwa virago, Kenneth Asamoah dakika ya 118 katika mechi iliyodumu kwa
saa mbili.
Yanga, leo
wanatetea taji dhidi ya timu ambayo inakuja juu kwa kasi ya kuridhisha katika
soka ya Tanzania, tayari kuingia kwenye orodha ya timu mpya tishio barani Afrika
kama Berekum Chelsea ya Ghana, Azam FC inayomilikiwa na mfanyabiashara Said
Salim Bakhresa.
Yanga
wataingia uwanjani, wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mechi tatu mfululizo za
mashindano na Azam msimu uliopita, mbili za Ligi Kuu na moja ya Kombe la
Mapinduzi na zaidi mbele ya mdomo wa lango lao, atakuwapo John Bocco ‘Adebayor’,
ambaye amekuwa na bahati ya kutikisa nyavu zao.
Lakini kwa
ujumla, tangu Azam ipande Ligi Kuu mwaka 2008, imekutana na Yanga mara 14,
imeshinda mara saba, sare tatu na kufungwa nne.
Ukuta wa
Yanga, utakaoongozwa na Kelvin Patrick Yondan, utakuwa na shughuli nzito ya
kukabiliana na viungo washambuliaji wa Azam wenye kasi kama Kipre Herman
Tchetche, ambaye kwenye mashindano ya mwaka huu amecheza kwa kiwango cha
juu.
Lakini ukuta
wa Azam utakaongozwa na Mwanasoka Bora wa Tanzania, Aggrey Morris utakuwa na
kibarua kizito cha kukabiliana na washambuliaji wawili wenye uchu, Said Bahanuzi
‘Spider Man’ na Hamisi Kiiza ‘Diego’, ambao kwa pamoja wameifungia Yanga mabao
10, matano kila mmoja hadi sasa sawa na Bocco.
Kocha wa
Yanga, Tom Saintfiet amesema kwamba fainali ya Kombe la Kagame itakuwa ngumu kwa
sababu wapinzani wao, Azam FC ni timu yenye kucheza kandanda ya kuvutia na
amesikitikia kuwa na majeruhi wengi kikosini.
Amesema
katika mchezo wa leo, atawakosa nyota wake wanne kati ya 20 aliowasajili kwa
ajili ya mashindano haya, ambao ni kipa Yaw Berko, mabeki Juma Abdul ambao ni
majeruhi, Godfrey Taita anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu na Nizar Khalfan
ambaye ni majeruhi pia.
Hata hivyo,
Mtakatifu Tom amesema kwamba pamoja na ukweli huo wanahitaji kutetea Kombe na
watapigana hivyo hivyo pamoja na changamoto zinazowakabili kuhakikisha taji
linabaki nyumbani.
Ikumbukwe
Yanga ilifuzu kuingia Fainali, baada ya kuifunga APR 1-0, bao pekee la mwanasoka
bora wa Uganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ dakika ya 110, akiunganisha krosi ya karibu
ya Haruna Niyonzima ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa APR kuzubaa
wakisikilizia maamuzi ya refa, baada ya Said Bahanuzi kuangushwa.
Wakati Azam
wanawania taji la kwanza kabisa la michuano hii, wanayoshiriki kwa mara ya
kwanza, Yanga watakuwa wakisaka taji la tano, baada ya awali kutwaa Kombe hilo
1975, 1993, 1999 na 2011.
Kocha
Muingereza, Stewart Hall wa Azam FC iliyoitoa AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC) ili kuingia fainali, kwa kuifunga mabao 2-1, mabao yake
yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, amesema kwamba Yanga ni
timu nzuri na fainali hiyo itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa.
Stewart
ambaye mapema mwaka huu aliiwezesha Azam kutwaa taji la kwanza, Kombe la
Mapinduzi, alisema kwamba Yanga imekuwa ikiimarika siku hadi siku na sasa
imefikia kuwa timu bora na anatarajia upinzani mkali leo.
Muingereza
huyo alisema kwamba pamoja na ukweli huo nia yao Azam ni kutwaa Kombe hilo.
“Vijana wangu hadi sasa wamenifurahisha kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yangu.
Mechi na AS Vita ilikuwa ngumu, hadi mapumziko tulikuwa nyuma kwa 1-0. Lakini
niliwaambia tukiwa vyumbani, watulie tuendelee kucheza mpira wetu, tusihamaki,
walinielewa na wakacheza nilivyotaka.
Hiyo ndio
siri ya ushindi, kwa kiwango kile na uchezaji ule, naona kabisa tunaweza
kuwafunga Yanga na kuchukua Kombe, timu yetu ni nzuri na wachezaji wanatulia
uwanjani kama ulivyoona,”alisema.
Stewart sasa
baada ya kuiwezesha Azam kuwa timu ya pili nje ya Simba na Yanga kuingia fainali
ya Kombe la Kagame, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo ilifungwa na Polisi
Uganda mabao 2-1, anafukuzia rekodi ya kuifanya Azam kuwa timu pekee nchini nje
ya vigogo hao, kutwaa taji hilo.
Katika
mchezo wa leo, vikosi vinatarajiwa kuwa;
Yanga
SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Haruna
Niyonzoma, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David
Luhende. Benchi; Shamte Ally, Juma Seif, Ladislaus Mbogo, Idrisa
Assenga na Jerry Tegete.
Azam
FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad,
Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tcheche, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’,
Ibrahim Mwaipopo na Ramadhan Chombo ‘Redondo’. Benchi; Mwadini
Ally, Samir Haji Nuhu, Joseph Owino, George Odhiambo, Mrisho Ngassa, Khamis Mcha
‘Vialli’ na Gaudence Mwaikimba.
Chanzo: BZ Blog
Post a Comment