Waasisi wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na Abeid Karume wakiufurahia Muungano
Na
Emmanuel J. Shilatu
Afrika haikuwa na mipaka ya nchi ndogo ndogo kama
ilivyo hii leo mpaka Wakoloni walipokuja na kuyagawa ambapo leo hii tunaita
nchi kupitia mkutano wao batili wa Berlin 1886 kwani hakuhusishwa Mwafrika
yoyote yule. Lengo kuu ni kuweza
kututawala kirahisi ambapo kukaibuka Tanganyika waliyopewa Wajerumani na
Zanzibar ikapewa Sultan wa Oman huku akisimamiwa na Waingereza. Sultan Oman
aliingia Zanzibar tangu 1832 kutokana na kuvutiwa na marashi ya Zanzibar.
Baada ya Mjerumani kushindwa vita vya kwanza vya
Dunia na Waingereza ilimfanya kupokonywa himaya zake, Tanganyika ikiwemo.
Hatimaye Watanganyika walipata Uhuru wao 9, Disemba 1961 kutoka kwa Waingereza,
nao wananchi wa Zanzibar walifanya mapinduzi ya kung’oa ruba ya utawala wa
kisultani 12, Januari 1964.
Ikumbukwe harakati za kulikomboa Bara la Afrika
miaka ya 1950 zilikuwa zikiongozwa na shujaa Kwame Nkurumah aliyejiwezesha nchi
yake ya Ghana kupata Uhuru wake mwaka 1957, hali iliyochochea nchi nyingine
kutafuta uhuru wao akiwa na lengo la kuleta na kujenga umoja wa nchi za Afrika
kwa mkupuo.
Lakini Mwalimu Nyerere akiwa na Mtazamo tofauti wa
kuiunganisha Afrika kwa awamu na alianzia na wazo la kuunganisha Afrika
mashariki. Jitihada zake ziligonga mwamba kwa Marais wa nchi hizo ambazo ni
Jomo Kenyata (Kenya) na Milton Obote wa (Uganda) ambao walikinzana kimtazamo na
Mwalimu.
Baadae Mwalimu alipata wazo lingine la kuziunganisha
Tanganyika na Zanzibar, na kwa awamu hii
Rais Abeid Karume (wa Zanzibar kwa kipindi hicho) alikubali wazo lake
ambalo hatimaye lilizaa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ni miaka 48 imepita tangu jahazi lililowabeba
Watanganyika na Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya
Jamhuri Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. Hii ilitokana
na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume (Zanzibar).
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa
kimazingira na mahusiano ambayo yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa
pande zote mbili (Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia,
kisayansi, kitamaduni na kihistoria
zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi
inaaminika kabisa kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana
na hata kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika.
Hivyo tangu awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya
pamoja.
Pia kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya Wakazi
wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa ilizidi
kushamiri baina yao.
Halikadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru
wetu ili tuweze kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia
kutuunganisha. Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya
Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa
Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa
kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar
kushiriki katika mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na
asilimia kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda
yake yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa
Gombani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na
ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na
hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo
Mwalimu Nyerere ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada
zake zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa
kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.
Mnamo April 22,1964, Maraisi wa nchi hizi mbili
ambazo sasa zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya
Tanganyika) na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia
sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya
Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar (URTZ).
Siku ya Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi
wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja
tu la kubadilishana “Hati za Muungano”.
Kutokana na kuyapiku majina ya Tangibar” na Tanzani
yaliyokuwa kwenye mchakato wa ushindano wa jina halisia litakalotumika , mnamo
tarehe 28 Octoba 1964, jina la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”
lilibadilishwa jina na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria
ya Jamhuri ya Muungano, sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Na tarehe 29 Oktoba, 1964 lilitangazwa rasmi jina la
Tanzania mbele ya Baraza la mawaziri wa serikali ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar na Mwalimu Julius Nyerere.
Neno TANZANIA linatokana na muunganiko wa herufi
TAN- kuwakilisha Tanganyika, ZAN- kuwakilisha Zanzibar, na herufi IA -zilichukuliwa kutoka kwenye Tanganyika na
Zanzibar kama viwakilishi vinavyokamilisha Muungano.
Pia tusisahau ya kuwa wananchi wa Tanzania walipiga
kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza kabisa wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.
Kama nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania
ulifikiwa kwa kutiwa sahihi mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa nchi hizi
mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) Aprili 22,1964
na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25,1964 na hatimaye kuwa sheria ya
Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na
ndiyo iliyopewa haki ya chombo cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za
Serikali ya Muungano.
Mwanzoni kabisa Hati ya Muungano (Articles of Union)
iliyomo ndani ya sheria ya Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya
Muungano. Mambo hayo ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama
(lakini si usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za
nchi za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi wa
fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati
ya Muungano imekuwa ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele
kwa malengo kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule
tulioanza nao awali na halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya Muungano
huu uendelee kudumu hadi hii kesho.
Ndio maana
mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea kuboreshwa kila
siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11 ambapo hii leo yamefikia
takribani 23.
Mengineyo ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama
vile;- Noti; Elimu ya juu,; Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa
za mafuta na gesi asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti;
utabiri wa hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979;
pamoja na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Interim Constitution of The United
Republic of Tanzania) mpaka kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya
kudumu ya jJamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi
sasa, ingawaje pia umeanzishwa mchakato wa kuandikwa mswaada wa mabadiliko ya
Katiba mpya.
Mwaka huo huo wa 1977 yaani miaka 13 baada ya
Muungano kutokea kulikuwa na muungano wa vyama vikubwa viwili kuungana kutoka
pande zote mbili (Bara na Visiwani). Vyama hivyo ni TANU (Tanganyika African
National Union) pamoja na ASP (Afro Shiraz Party) cha Zanzibar kuungana na
kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) .
Hatua ama vitendo na mafanikio hayo si tu kwamba
yalidumisha bali hata yaliendeleza kukuza Muungano wetu ambao Jahazi lake
liligubikwa na misukosuko ya mawimbi makubwa baharini uliojaa uzito wa mambo
mbalimbali uliokuja kwa sera ya kero zilizoleta chokochoko mbalimbali katika
Muungano wetu., ambao hatutakiwi kamwe kuusahau maishani mwetu.
Tusisahau mchezo mchafu uliojaa rafu za kutisha
uliotaka kufanywa na Bunge miaka ya 1990 na 1992 ya kutaka kuyakubali madai
yaliyotolewa na kundi la G55 ambalo
lilitaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika , hali hii ingetuvuruga kwani
ilihitaji uwepo na serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika yatupasa
tuzishukuru hekima na busara za Mwalimu Nyerere kwa kutuokoa na chokochoko ya
kero hii.
Pia
tusiisahau kero ama chokochoko nyingine ya Muungano wetu iliyoibuka Decemba 1,
1992, ambayo Zanzibar ilitaka kujiunga na umoja wa Nchi za Kiislam Duniani
(OIC) kama nchi nje ya Muungano.
Tuendelee kukumbuka ni kwa jinsi gani Zanzibar
iliyokuwa inasaka ukuu nje ya Muungano kwa kuibua madai ya Bendera ya Taifa
lake (Zanzibar), wimbo wa Taifa, na nembo yao ya Taifa.
Kwa nyakati tofauti tofauti tumekuwa tukisikia baadhi
ya Wazanzibari walio wachache wakiilalamikia hali nzima ya ongezeko la mambo
kwenye Hati Muungano (Articles of Union) kutoka mambo 11 hadi kufikia 23 ambalo
ni sawa na ongezeko la mambo 12 ambao kwa baadhi yao hawaoni umuhimu wa wa
uwepo wake na hata kutishia kujitoa. Ila asilimia kubwa ya Wazanzibari
wanayaunga mkono, hali iliyo sababisha hoja ya wachache kuzidiwa nguvu.
Pia tumekwisha sikia jinsi gani Wazanzibari
wanavyotaka jambo la maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na aina
nyingine za mafuta au bidhaa na gesi asilia iondolewe katika masuala ya
Muungano ili Zanzibar ipate kunufaika zaidi na maliasili zake.
Kukuru kakara za Wazanzibari zinatookana na madai
yao ya kuwa Tanganyika(Bara) imeimeza Zanzibar (Visiwani) katika masuala mazima
yahusuyo Muungano. Ikumbukwe Ubaguzi wa dhana ya Tanganyika umeimeza Zanzibar
si ya kweli na hii imebainishwa katika katiba ya Muungano kuwa kuna Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Haya ni mapenzi ya dhati waliyoonyesha kwa
Wazanzibari kwa kuwaruhusu wawe na serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ikumbukwe Serikali ya Muungano inaongozwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaongozwa na Baraza la
Mapinduzi ya Zanzibar na chombo chao cha kutunga sheria kinaitwa Baraza la
Wawakilishi.
Ndugu zangu hali ya kupuuzia na hata kuuchezea
Muungano wetu ni hatari sana tena ni dhambi iliyotukuka. Mathalani Wazanzibari
wakiamua kujiengua kwenye huu Muungano ili wawe kivyao vyao,hawatabaki salama.
Mwalimu Nyerere alishawahi kusema ya kuwa “wakifika kwenye hatua hiyo
watagundua kuwa ndani yao kuna Wazanzibari na Wazanzibara”. Nao wataamua
kuwafukuza wale wa Wazanzibara, lakini hiyo haitakuwa mwisho. Punde si punde
watajigundua kuwa nao (Wazanzibari) wamegawanyika kwani kuna Wapemba na
Waunguja, na wakifikia hapo pia hawatakuwa salama ni lazima machafuko
yatatokea.
Daima Wazanzibari watambue ya kuwa dhambi ya
kutokutamalaki kwa dhana ya Unguja na Pemba unatoka na kufunikwa na kivuli cha
mwamvuli cha Muungano. Hivyo umoja, mshikamano, amani na utulivu wao unategemea
sana uwepo wa nguzo hii imara ya Muungano huu tulionao.
Vivyo hivyo kwa watu wa Bara (Tanganyika) ni rahisi
kwao kutafunwa na dhambi ile ile ya ubaguzi watakayo ianzisha nje ya uwepo wa
Muungano ni rahisi sana kwa ukabila, udini, ukanda na hata U-rangi kutamalaki
ndani ya jamii wakishafikia hapo, hawatabaki salama kwani watachafuana tu.
Muungano huu tulionao unawafanya wale wageni,
mataifa ya nje na watu wote wenye hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa
na kutuvuruga kutokana na kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na
mshikamano baina yetu.
Muungano huu
wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe ni bara ama
ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda Visiwani na hata
wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru huo wa uwepo wa nafasi
hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.
Kutokana na uwepo wa uhuru wa kusafiri usio na
mipaka baina yetu, pia Muungano wetu tulionao unazidi kutuongezea fursa na
nafasi zaidi ya uwanja mpana wa ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo
wa mzunguko mkubwa wa pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa
zikitoka Visiwani (Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya
bidhaa kama vile nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka
Bahari na kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa
biashara kama vile Magari, nazi, Karafuu, Tende na kadhalika.
Ndugu zangu, mpaka sasa natafuta jibu na bado
sijalipata la huu Muungano wetu una ubaya gani kwetu? Muungano huu tulionao ni
nguzo ya uwepo wa umoja,mshikamano, amani na utulivu hapa nchini ;Muungano wetu
hautunyimi fursa ya kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, ama kutoka
himaya moja kwenda himaya nyingine; Muungano huu hautukatazi kabisa nafasi ya
mwingiliano baina ya tamaduni moja na tamaduni nyingine bila ya kujurisha ni wa
Bara ama Visiwani
Muungano huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja
mpana tena usio na kikomo wa ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama
kutojulisha au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za
kijamii bora, Muungano hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano
sahihi wa upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya
Muungano” (Articles of union). Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha
mzima wa nyanja za kimaisha yetu. Tatizo la huu Muungano wetu ni lipi haswa?
Ni ukweli uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano
kama huu (wa Tanganyika na Zanzibar)
hapa Barani Afrika umoja ushirikiano, ushikamano, amani na utulivu ni sehemu
mojawapo ya manufaa ya Muungano huu.
Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu ni kwa
kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake waliotuachia. Watanzania
yatupasa tuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwani ni
nguzo na fahari ya kipekee na ya aina yake Barani Afrika. Naomba kutoa
hoja
Post a Comment