MKURUGENZI wa shirika la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) Kanali Ayoub
Mwakang’ata na maofisa wenzake sita wa jeshi hilo jana walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka saba ya
kula njama na matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na Kanali Mwakang’ta washtakiwa wengine ni Luteni kanali Mkohi Kichogo,
Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajenti John lazier, Meja Yohana
Nyichi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta wa SUMA JKT-Luteni Kanali Felex
Samillan.
Mawakili toka ofisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU), Dominsian
Kessy na Ben Lincoln, walidai mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana katika kosa
la kwanza maafisa hao wote wanashtakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kinyume
na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Wakili Kessy alidai kuwa Machi 5, 2009 katika chumba cha mikutano cha ofisi
ya SUMA JKT Dar es Salaam, wakiwa ni wajumbe wa bodi na Bodi ya Tenda ya SUMA
JKT kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa maamuzi ya bodi hiyo
ambayo yalionyesha yametolewa na TAKOPA kwa madhumuni ya kununua magari na vifaa
vya ujenzi bila kupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi ya TAKOPA.
Wakili Kessy alidai kosa la pili pia ni la matumizi mabaya ya madaraka ambalo
linawakabili washtakiwa wote kuwa Machi 12, 2012 , washtakiwa hao wakiwa ni
wajumbe wa bodi ya Tenda ya SUMA JKT walitumia madaraka yao vibaya kupitishia
maazimio ya kununuliwa kwa magari na vifaa vya ujenzi ambavyo vilikuwa
vimeishatumika kinyume na kifungu cha 58( 3) cha Sheria ya Mamunuzi ya Umma ya
mwaka 2005.
Aidha shtaka la tatu ni la matumizi mabaya ya madaraka linalomkabili
mshtakiwa wa pili na wa saba (Kichogo, Samillan) ambapo Machi 16, 2009 wakiwa
wajumbe wa bodi ya Tenda ya SUMA JKT wanadaiwa kuhamisha Sh 2,744,432,545
kupitia hundi Na.000010 kutoka akaunti ya TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT
akaunti Na.01110307094 ambazo zote zipo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kufuata
matakwa ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha ya Umma na Kanuni zake ya mwaka
2001.
Shitaka la nne alidai linalowakabili washitakiwa wa pili na watatu ambalo pia
ni la matumuzi mabaya ya madaraka wanalodaiwa kulitenda Aprili 3 mwaka
2009,wakiwa wajumbe wa bodi hiyo ambapo walihamisha sh milioni 489,677,879.30
kupitia hundi Na.000011 kutoka TAKOPA akaunti Na.011103031763 kwa akaunti Na.
011103017094 ya SUMA JKT bila kufuata kanuni na matakwa ya kifungu cha 156 cha
Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001.
Shitaka la tano ambalo linawakabili tena washitakiwa hao wawili ni matumizi
mabaya ya madaraka ambapo inadaiwa Aprili 4 mwaka 2009 wakiwa ni wajumbe wa bodi
hiyo walihamisha Sh 269,519,093.60 kupitia hundi Na.000012 kutoka akaunti ya
TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT akaunti Na.011103017094 bila kuzingatia
masharti ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha za umma na kanuni zake ya mwaka
2001.
Katika shitaka la sita linalowakabili washitakiwa hao wawili tena pia ni la
matumizi mabaya ya madaraka ambapo Mei 4 mwaka 2009 wakiwa ni wajumbe wa bodi
hiyo, walihamisha shilingi 350,000,000,000 kupitia hundi Na.000015 kutoka
akaunti ya TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT akaunti Na. 011103017094 bila
kufuata matakwa ya kifungu hicho cha sheria ya fedha za umma.
Hata hivyo alidai shitaka la saba linawakabili washitakiwa wote ambalo ni la
kula njama kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
ya mwaka 2007, ikidaiwa kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2009 wakiwa wajumbe wa
bodi hiyo jijini Dar es Salaam, walikula njama na kuhamisha mradi kutoka akaunti
ya TAKOPA Na. 011103017094 bila kufuata matakwa ya kifungu cha 156 cha Sheria ya
Fedha ya umma na kanuni zake ya mwaka 2001.
Hata hivyo washitakiwa wote walikana na Hakimu Katema aliwaachia kwa dhamana
baada ya kila mmoja kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika
ambao watasaini bondi ya sh milioni 25 kila mmoja. Kesi imeahirishwa hadi Agosti
Mosi huu, itakapotajwa tena.
chanzo: Tanzania Daima |
Post a Comment