Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya 2012 yaliyofanywa na Bunge yamezua mtafaruku na sintofahamu, huku wafanyakazi wa sekta mbalimbali wakiyapinga kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga kuwanyima haki ya fedha wanazokatwa kwa mujibu wa sheria kuchangia mifuko hiyo. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicolaus Mgaya aliliambia gazeti hili jana kuwa, watafungua kesi katika Mahakama ya Kazi nchini, kupinga hatua ya Serikali kubadili Sheria ya muda wa lazima wa kuchukua mafao hayo ambao ni kati ya miaka 55 na 60. Tangu juzi watu kutoka sehemu mbalimbali hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakipiga simu katika chumba cha habari cha Mwananchi kwa lengo la kupata ufafanuzi wa mabadiliko hayo ya sheria yaliyopitishwa na mkutano wa saba wa Bunge, Aprili 13 mwaka huu. Kadhalika sheria hiyo inayozuia mwanachama wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii kuchukua mafao kabla ya umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ambao ni miaka 55, lilichukua nafasi kubwa katika mijadala ya mitandao ya kijamii ambako wengi wa wanaliochangia, wameiponda sheria hiyo na kuiita kuwa ni ya ‘kinyonyaji’. Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka alisema jana kuwa: “Hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi, maana sheria hii itafuatiwa na kanuni na miogozo mingine ambayo ninaamini kwamba itaondoa wasiwasi uliopo”. Isaka alisema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika miongozo hiyo ni iwapo mwanachama atafukuzwa au kuachishwa kazi, wanachama ambao wako kwenye kazi za mikataba na wale wanaopata ulemavu wa kudumu wakiwa kazini. “Kimsingi ni kwamba suala la mafao ya kuacha kazi kabla ya umri wa kisheria wa kustaafu limefutwa kwa mifuko yote, isipokuwa katika mazingira hayo niliyoyaeleza litawekewa miongozo, na hii ni kwa faida ya wachangiaji,”alisema Isaka. Alisema baada ya sheria hiyo kuwa imepitishwa na Bunge, kisha kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Juni mwaka huu, SSRA ilianza mchakato wa kuweka miongozo na baada ya hapo kinachofuatia ni kutoa elimu kwa umma na baadaye kuanza kutumika kwake rasmi. “Lakini sasa tumelazimika kuanza kutekeleza sheria hiyo mapema kuliko tulivyopanga hasa baada ya kutokea kwa suala hili kwenye public (umma) kabla ya muda tuliokuwa tumekusudia,”alisema mkurugenzi huyo. Isaka aliongeza kuwa chimbuko la sintofahamu iliyojitokeza ni baadhi ya mifuko kuchezeana rafu kwa lengo la kupata wanachama wapya kwenye migodi na kwamba wao kama wadhibiti tayari wametoa onyo kwa mifuko iliyohusika. “Kwanza hakuna mfuko wowote ambao una mamlaka ya kutangaza kuanza kutumika kwa sheria, ni SSRA tu wenye mamlaka hayo, kwa hiyo tumewapa onyo, kama wanajitangaza wajitangaze kwa kueleza uzuri wa mfuko wao ni siyo kuchafuana au kuchafua wengine,” alisisitiza. Wasemavyo wafanyakazi Mgaya alisema sheria hiyo ni kandamizi kwani inamnyima fursa mfanyakazi aliyestaafu au kufukuzwa kazi kupata malipo yake ambayo ni halali. “Sheria hii sisi hatuikubali na tunaipinga kwa nguvu zote na tutakwenda Mahakama ya Kazi kufungua kesi ya kupinga kutumika,” alisema Mgaya na kuongeza: “Tutafanya mawasiliano na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuwaeleza kuhusu sheria hii ili watusaidie na ikishindikana azma yetu ni kwenda mahakamani.” Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba haiwezekani mtu anafukuzwa kazi akiwa na miaka 45 na baadhi yao hawataki tena kuajiriwa wanataka kufanyabiashara halafu unamnyima mafao yake hadi afikishe miaka 55, kitu ambacho kitamfanya mtu huyo aishi maisha magumu. “Sheria hiyo ingekuwa na usawa ingetumika kwa wafanyakazi wote wa Serikali na kutowabagua kama inavyojieleza kwamba, Mbunge akimaliza miaka yake mitano anachukua mafao yake. Sasa kwa nini iwe kwao tu na si kwetu pia?,” alihoji Mgaya. Kwa upande wao Chama cha Wafanyakazi wa Migodini (Tamico) Wilaya ya Geita, kimesema kitapeleka maombi maalumu kwa Rais Kikwete kupinga marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Katibu wa Tamico Wilaya ya Geita, Benjamin Dotto alisema wameamua kupiga kura ya maoni juu ya mabadiliko ya sheria hiyo, ili wanachama wao waamue wenyewe kama wanaitaka au la. ”Tunamwomba Rais aagize kupelekwa muswada wa marekebisho bungeni, kwa ajili ya kipengele ambacho kimeleta mtafaruku,” alisema Dotto. Alisema kipengele cha kuzuia mfanyakazi kuchukua mafao yake hadi afikishe umri wa miaka 55, kinakandamiza masilahi ya mfanyakazi mnyonge ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akichangia mapato ya nchi kupitia kodi anayokatwa. Chimbuko la sheria Mabadiliko ya sheria hizo za mifuko ya hifadhi ya jamii yalifanywa na Bunge Aprili 13 mwaka huu, baada ya muswada husika kuwa umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni Februari 1, 2012. Ibara ya 107 ya muswada huo ndiyo ilipendekezwa kufutwa kwa Ibara za 37 na 44 za Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) ambavyo vilikuwa vikiruhusu mafao ya kujitoa. Meneja uhusiano wa SSRA Sara Mssika alisema jana kuwa kufutwa kwa ibara hizo kulimaanisha kwamba hakuna mfuko wowote unaoruhusiwa kutoa tena mafao ya aina hiyo hadi hapo miongozo mipya itakapotolewa. “Hakuna sheria ya mfuko mwingine iliyokuwa ikiruhusu mafao ya kujitoa, na kama wapo waliokuwa wakifanya hivyo, basi walikuwa wanafanya hivyo pengine kwa taratibu nyingine ambazo ni nje ya sheria za kuanzishwa kwa mifuko yao,”alisema Mssika. Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka akiwasilisha maelezo ya muswada huo bungeni alisema lengo la marekebisho katika Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuiwezesha SSRA kufanya kazi yake kikamilifu na kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii. Alisema muswada huo uliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, wakiwamo wafanyakazi, waajiri na Serikali, pia mifuko yenyewe kupitia vikao vya wadau na Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi Jamii na Uchumi. “Kimsingi, wadau wote waliunga mkono mapendekezo yaliyomo katika muswada huu,” alisema Kabaka na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yatawezesha kupanuliwa kwa wigo wa wanachama kwenye mfuko kwa kuruhusu wafanyakazi wanaoingia kwenye ajira kwa mara ya kwanza ama kujiajiri wenyewe ili waweze kujiunga. chanzo: Mwananchi |
Loading...
Sheria mpya mifuko ya jamii yazua mtafaruku nchini
BLOG RAFIKI
-
-
-
-
-
-
Jioni11 hours ago
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
-
Post a Comment