Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imetoa taarifa usiku huu ikieleza idadi ya watu
waliopatikana wakiwa hai ni 146 na kupata maiti 62.
Akitoa
taarifa hiyo kwa vyombo vya habari usiku leo,Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Amali Ali Juma Shamuhuna alisema taarifa hiyo ndio sahihi na
kuwataka wananchi kutoamini taarifa zinazotolewa na watu wengine zaidi
ya Serikali.
Waziri
Shamuhuna alisema kwamba maiti 62 walipatikana ambao kati ya maiti hizo
watoto ni 9 na kuna raia mmoja wa kike wa kigeni ambaye hakuweza
kutambulika Uraia wake,lakini umeonekana picha yake moja ndogo ya hati
ya kusafiria.
Waziri Shamuhuna alisema meli hiyo ilibeba jumla ya abiria 290 kati ya hao watu wazima 250, watoto wadogo 31 na mabaharia 9.
Waziri
huyo aliwataka wananchi katika sehemu mbalimbali hasa katika vijiji
vilivyo kandokando ya bahari watakapoona maiti au mtu akiwa hai ambaye
wanadhani ni wa ajali ya Meli ya Skagit.
Aidha,
Waziri Shamuhuna alisema kwamba kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
ambao watakuwa na wasiwasi wa kutowaona ndugu na jamaa zao amewataka
kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kupata
taarifa zaidi au kuripoti habari za kupotelewa kwa ndugu au jamaa zao.
Kwa upande wa Zanzibar, Waziri huyo aliwataka wananchi kufika kwa Masheha wao kutoa taarifa kama hizo.
Serikali
imewashukuru makampuni binafsi za usafiri baharini kwa msaada wao na
wasisite kutoa msaada katika kazi inayoendelea ya kutafuta watu au maiti
wengine katika eneo la tukio.
Meli
ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 karibu na Kisiwa cha Chumbe umbali
wa maili sita kuelekea Kusini mwa Kisiwa kidogo cha Yasin Zanzibar
ikitokea Bandari ya Dar es Salaam ilikoanza safari saa 5:30 asubuhi.
Meli
hiyo inamilikiwa na Kampuni ya Sea Guall Sea Transport Ltd, Kampuni
ambayo Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilizama ikiwa Bandarini Malindi
Zanzibar na kufariki watu sita mwaka 2009.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
ZANZIBAR, TANZANIA
JULAI 19,2012
Post a Comment