Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Agrey Mwanri
|
|
|
SERIKALI imesema suala la watumishi kuchelewa kurekebishiwa mishahara yao
baada ya kupandishwa vyeo umechangiwa na utaratibu uliokuwepo ambao ulikuwa
ukimtaka mtumishi kukubali kwanza baada ya kupewa barua ya kupanda cheo.
Hayo yalibainishwa mjini hapa jana na Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Waziri
mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Agrey Mwanri wakati
alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalum Rachel Robert
(CHADEMA) aliyetaka kujua ni kwa nini serikali haitekelezi maelekezo yaliyomo
kwenye barua za watumishi wanaopandishwa vyeo wakati watatekeleza majukumu yao
kwenye cheo alichopandishwa.
“Kumekuwepo na utaratibu wa Manispaa zetu nchini kuwapandisha vyeo waajiriwa
wake wakiwemo wauguzi wakiwapa barua na maelekezo yote yapasayo ya upandishwaji
vyeo hivyo lakini (kamwe utekelezaji wa yale yaliyoelekezwa kwenye barua zao
hayafanyiki pengine muda mrefu sana na hata zaidi ya miaka miwili bila
utekelezaji,” alisema mbunge huyo.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri huyo alisema awali mtumishi
alitakiwa kukubali kwanza baada ya kupokea barua ya kupandishwa cheo na ndipo
mwajiri wake aziwasilishe ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Alisema kwa sasa Serikali imechukua hatua madhubuti katika kushughulikia
suala hilo kwa kusimika mfumo wa kieletroniki wa taarifa za utumishi (Human
Capital Information Management System-LAWSON Version 9) katika halmashauri.
Mwanri alifafanua kuwa maafisa rasilimali watu wamepatiwa mafunzo ya kutumia
mfumo huu ambapo barua za kupandishwa cheo hutumwa kwa kutumia mfumo huo.
“Hivyo, malipo ya mishahara sasa yanafanyika ndani ya muda mfupi baada ya
mtumishi kupandishwa cheo, kwa mfano taarifa za mtumishi zinatakiwa kabla ya
tarehe tano (5) mtumishi atapokea mshahara mpya ndani ya mwezi huu,” alisema
Naibu Waziri huyo.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri huyo alitoa wito kwa halmashauri kuzingatia
na kutumia mfumo huu kikamilifu ili kuepuka malimbikizo ya madeni ya watumishi,
mara mtumishi anapopandishwa cheo taarifa ziingizwe katika mfumo na kutumwa
mapema iwezekanavyo.
chanzo: Tanzania Daima
|
|
on Wednesday, July 11, 2012
Post a Comment