Alex Mgongolwa |
Na Bongostaz
KIKAO cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, kilichofanyika
Julai 17, mwaka huu, kupitia mikataba na nyaraka zote zinazohusiana na mchezaji
Kevin Yondani katika kujiridhisha juu ya hadhi yake ya usajili katika
mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kimemhalalisha
beki huyo wa kati kuchezea Yanga.
Taarifa ya Mwenyekiti Kamati hiyo ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), imesema;
“1. Kwa mujibu wa
mapitio ya nyaraka zote zilizotajwa hapo juu na kufanyiwa upembuzi yakinifu,
Kamati iliridhika pasi na shaka yoyote kuwa suala zima la mchezaji Kevin
Yondani ni la kiutendaji, hivyo uamuzi wa Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na
Klabu ya Simba kwa suala hilo la kiutendaji
kama Sekretarieti ilivyofanya
katika barua yake ya Julai 14 mwaka huu ulikuwa sahihi.
2. Kamati ilibaini
kuwa Mkataba wa mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya Simba ulimalizika Mei 31
mwaka huu. Hivyo kwa taratibu za usajili mchezaji Kevin Yondani kuanzia Juni 1
mwaka huu alikuwa ni mchezaji huru.
3. Aidha Kamati
ilibaini kuwa Mkataba uliowasilishwa na Klabu ya Simba TFF ukiwa na maana ya
kuongeza mkataba uliokuwepo TFF baina ya mchezaji Kevin Yondani na Klabu ya
Simba uliwasilishwa TFF, Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa
kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya kuongeza
muda wa mikataba ya wachezaji wao wakati mkataba halisi haujaisha muda wake.
Hivyo mkataba huo kwa jicho la kisheria haupo.
4. Hata kama kamati
ingeuona mkataba huo katika jicho la sheria, bado mkataba huo una tatizo la
kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano
hayo. Ukiuangalia mkataba huo unabainisha kuwa, wakati mchezaji Kevin Yondani
aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao
ni Klabu ya Simba inaonekana iliingia makubaliano hayo kupitia kwa Makamu
Mwenyekiti wake Geofrey Nyange Kaburu, Desemba 23 mwaka huu.
5. Kisheria utata
huu unaweza kuondolewa na pande husika tu kwa kurekebisha dosari hiyo kwa
maridhiano kuweka saini katika mabadiliko hayo ili kuthibitisha mabadiliko
hayo. Hivyo katika jicho la kisheria mkataba huo hauwezi kutumika kumzuia
mchezaji huyo kwenda katika klabu anayoipenda wakati akiwa huru.
Kutokana na maelezo yote hapo juu, Kamati imeridhia hatua
iliyochukuliwa na Sekretarieti ya TFF ya kumruhusu mchezaji Kevin Yondani
kuichezea timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Kagame 2012,”
Post a Comment