Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

ASKOFU KIKOTI AFARIKI DUUNIA





Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda mkoani Katavi, Dk Paschal William Kikoti (55)
Waandishi Wetu
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mpanda mkoani Katavi, Dk Paschal William Kikoti (55), amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu katika Hospitali ya Bugando, Mwanza.

Makamu Askofu wa jimbo hilo, ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Karema na Mwambao wa Ziwa Tanganyika, Padri Patrick Kasomo alitangaza kifo hicho juzi usiku kwenye kanisa kuu jimboni humo mbele ya waumini.
Alisema Askofu Kikoti alifariki dunia baada ya kupatwa ghafla na ugonjwa huo Jumapili iliyopita saa moja asubuhi wakati akioga baada ya kuanguka, kisha kupoteza fahamu.

Alisema aligunduliwa baadaye na mapadri na watawa waliotoka kwenye ibada ya misa ya kwanza saa mbili na nusu asubuhi.
Kutokana na tukio hilo, Padri Kasomo alisema uongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ulitafuta usafiri wa ndege siku hiyohiyo na kumsafirisha hadi Bugando kwa matibabu zaidi.
Alisema marehemu Askofu Kikoti alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu ambalo lilipanda kufikia 240 hadi 260, hali iliyomsababishia kifo.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, waumini wa kanisa hilo waliangua kilio na baadhi yao kupoteza fahamu.
Taarifa za awali zilieleza kuwa askofu huyo katika siku za karibuni aliwahi kusumbuliwa na homa.
Hadi jana, baadhi ya wageni mashuhuri walikuwa wameanza kuwasili jimboni humo ikiwa ni pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo la Tabora, Paul Ruzoka na mwenzake wa Jimbo la Sumbawanga, Damiano Kyaruzi.

Hospitalini Bugando
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Charles Majinge alisema kwa simu jana kwamba taarifa ya daktari aliyekuwa akimhudumia jimboni kwake inaeleza kuwa askofu huyo alianguka akiwa bafuni wakati akioga kutokana na shinikizo la damu ambalo lilimsababishia kiharusi.

“Baada ya kufikishwa hapa (Bugando), tulianza kumhudumia kwa saa 48 ili kuokoa maisha yake, lakini usiku wa kuamkia jana (juzi), saa mbili usiku aliaga dunia,” alisema Dk Majinge.

Msemaji wa Jimbo Kuu la Mwanza, Padri Christopher Kubeja alisema: “Kwa vile aliyefariki siyo askofu wa jimbo letu, hatuwezi kumzungumzia, ila ni kweli amefia Bugando alipokuwa akitibiwa.”
Alisema hivi sasa wanandaa misa ya kumwombea marehemu ambayo itafanyika leo saa 6:00 mchana katika Kanisa Kuu la Epifania, Bugando.

“Baada ya misa hiyo, saa 8:00mchana tutauondoa mwili wake Bugando na kuupeleka Uwanja wa Ndege wa Mwanza tayari kwa safari ya kwenda jimboni Mpanda,” alisema Padri Kubeja na kuwaomba waumini wote kujitokeza kwa wingi katika misa hiyo.

Taarifa ya TEC
Katibu Mkuu wa TEC, Padri Antony Makunde mbali ya kuthibitisha kuwapo kwa misa hizo, alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili Mpanda leo jioni na kwamba kanisa limetenga siku ya leo na kesho kwa waumini wa dini hiyo, ndugu jamaa na marafiki kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.Alisema mazishi ya Askofu huyo yamepangwa kufanyika Jumamosi na katika Kanisa Kuu la Mpanda.

Historia yake
Askofu Kikoti alizaliwa Machi 3, 1957 huko Ihimbo, Parokia ya Nyabula, Jimbo Katoliki la Iringa.
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Iringa, kisha elimu ya sekondari katika Seminari ndogo ya Mafinga na mafunzo ya falsafa katika Seminari ya Peramiho, Songea pamoja na Seminari Kuu ya Ntungamo, Bukoba.

Kwa upande wa theolojia, alisoma Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora na mwaka 1988 alipata daraja la upadri.
Baada ya upadrisho wake, alifanya kazi jimboni Iringa na kati ya mwaka 1989- 1990 alikwenda masomoni Rome, Italia ambako alisomea Historia ya Mababu wa Kanisa na Theolojia na kupata Udaktari wa Falsafa (PhD).

Mwaka 1997alirudi nchini na kufundisha katika Seminari ya Peramiho na Novemba 4, 2004, aliteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Mpanda na alisimikwa rasmi Januari 14, 2001 hadi umati ulipomfika.
Pia, alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi ya TEC tangu mwaka 2009 akisaidiwa na Katibu Mtendaji, Padri Raphael Madinda.

*Imeandikwa na Kibada Kibada, Mpanda, Sheilla Sezzy, Mussa Mwangoka, Ndyesumbilai Florian na Geoffrey Nyang’oro. CHANZO: MWANANCHI


Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top