Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia
kifo cha Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Baba Askofu
William Pascal Kikoti.
Kifo cha Askofu Kikoti kilitokea jana Jumanne tarehe 28 Agosti, 2012
katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mkoani Mwanza alikokuwa amelazwa
kwa matibabu kutokana na ugonjwa wa Shinikizo la Damu.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa
za kifo cha Baba Askofu William Pascal Kikoti wa Jimbo Katoliki la
Mpanda akiwa bado na umri mdogo wa miaka 55 wakati ndiyo kwanza utumishi
wake ulikuwa ukihitajika zaidi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu
zake na kuongeza,
“Ni dhahiri kwamba kifo cha Baba Askofu Kikoti kimeacha pengo kubwa la
kiuongozi siyo tu kwa Kanisa Katoliki hapa nchini, bali pia Jumuiya ya
Waamini wa Kanisa hilo kote duniani”.
Rais Kikwete amesema anatambua jitihada kubwa za Marehemu Baba Askofu
William Pascal Kikoti enzi za uhai wake katika kuwatumikia Waumini wa
Kanisa lake, na hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, tangu alipopata
Daraja la Upadre mwaka 1988, kuteuliwa kwake kuwa Askofu wa Kwanza wa
Jimbo Katoliki la Mpanda mwaka 2000, na hatimaye alipowekwa Wakfu na
Kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo mwaka 2001.
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Baba Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Salamu zangu
za Rambirambi, na kupitia kwako kwa Kanisa Katoliki na kwa Waumini wote
wa Kanisa hilo hapa nchini hususan wa Jimbo Katoliki la Mpanda, kwa
kumpoteza mmoja wa Viongozi muhimu na wa ngazi ya juu wa kiroho,
Marehemu Baba Askofu William Pascal Kikoti”, ameongeza kusema Rais
Kikwete.
Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzishe mahala
pema peponi Roho ya Marehemu. Amewahakikishia wote waliofikwa na msiba
huo kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa
kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2012
Post a Comment