BAADA ya kupokea taarifa za ugonjwa mpya
wa mahindi kutokea Kenya, Serikali imewataka wadau wote wa kilimo
kuhakikisha mbegu hizo kabla hazijaingizwa nchini, sampuli nilazima
ichukuliwe na kupelekwa kituo cha karantini cha ‘Tropical Pesticide Research Institute, (TPRI), kilichopo Arusha kwa ajiri ya kuzihakiki ili kuthibiti ugonjwa huo kuingia nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya
habari jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mohamed
Muya, ilieleza kuwa wamepokea taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania nchini
Kenya na Shirika la Kilimo na Chakula (Food and Agriculture Organization), juu ya kuwepo ugonjwa huo wa mahindi unaojulikana kwa jina la ‘Maize Lethal Necrotic Disease (MLND)’ ambapo ugonjwa huo unasababishwa na virusi vinavyojulikana kitaalamu “Maize Chlorotic Mottle Virus (MCMV)” na “Sugarcane Mosaic Virus (SCMV)”.
Alisema , ugonjwa huo ulianzia katika eneo la Bomet
lililopo katika Bonde la Ufa ambapo ulisababisha asilimia 100 ya
uharibifu wa zao la mahindi lililokuwepo shambani.
Muya alisema kulingana na taarifa hiyo, hadi sasa ugonjwa
huo umesambaa katika eneo kubwa ndani ya bonde la ufa na umeenea katika
wilaya 22 ambapo jumla ya hekta 16,000 za zao la mahindi zimeathirika
ambapo hasara kutokana na ugonjwa huo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia
60 hadi 90.
Alibainisha kuwa Ili kukabiliana na hatari ya uwezekano wa
ugonjwa huo kuingia nchini Tanzania, Wizara inawaarifu wadau wote wa
kilimo nchini kuzingatia maelekezo kutoka kwa wataalam.
Muya alisema kwa kuwa ugonjwa huo unaenezwa na mbegu,
Tanzania inaagiza kiasi kikubwa cha mbegu kutoka nje ya nchi, vibali
vyote vinavyotolewa kuingiza mbegu hizo lazima ziwe hazina vimelea vya
“Maize Lethal Necrotic Disease’ baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa
maabara.
Aidha, Halmashauri za Wilaya kwa kushirikiana na Wizara ya
Kilimo Chakula na Ushirika zinapaswa kutatoa elimu ya jinsi ya kutambua
ugonjwa huo na mbinu za kukabiliana nao.
Vilevile wakuu wote wa Mikoa, Wadau wote wa mbegu,
wakulima na wananchi kwa ujumla katika mikoa inayolima mahindi kwa
kutegemea umwagiliaji au kilimo cha msimu cha kutegema mvua wanapaswa
kutoa taarifa mapema endapo dalili zisizo za kawaida zitaonekana katika
mashamba ya mahindi.
Muya aliwashauri wakulima wote kuhakikisha kuwa wananunua mbegu zilizothibitishwa ubora na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (Tanzania Official Seed Certification Institute – TOSCI).
Sambamba na agizo hilo, wauzaji
na wasambazaji wa mbegu nchini wanaagizwa kuzingatia Sheria ya Mbegu ya
Mwaka 2003, kinyume chake watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Muya alitoa
wito kwa wananchi wote waliopo mipaka kutokuhamisha au kubeba mahindi
kiholela kutoka nchi jirani bila kufuata taratibu za kisheria.
Post a Comment