Simba,leo wameendeleza
wimbi lao la ushindi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya
kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, ushindi huo
ulipatikana huku timu hiyo ikiwa pungufu baada ya mshambuliaji wao
Mganda Emmanuel Okwi kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 38
baada ya kumpiga kiwiko beki wa JKT Ruvu, Kessy Mapande.
Pamoja na kumiliki vyema mpira
sehemu kubwa ya mchezo huo, JKT Ruvu walishindwa kabisa kuhimili
vishindo vya Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)
kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager, baada ya kujikuta ikilambwa mabao
hao mawili.
Kwa ushindi huo wa pili mfululizo
kwenye uwanja wake wa nyumbani, Simba imefanikiwa kufikisha pointi sita
na hivyo kuwa kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu
14.
Kiungo mkabaji Amri Kiemba, ndiye
aliyekuwa wa kwanza kuipatia Simba bao katika dakika ya 47 baada ya
shambulizi kali ambapo mabeki wa JKT Ruvu walishindwa kuwa makini
kuondosha hatari.
Katika dakika ya 72, Haruna Moshi
‘Boban’, aliipatia Simba bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka
kwa Mrisho Ngassa ambaye katika mchezo huo, alionekana kuwa mwiba mkali
kwa JKT Ruvu.
Wakati huohuo huko mkoani
Morogoro mji kasoro bahari timu ya Yanga pia ya jijini Dar es salaam
imechezea kichapo cha magoli 3-0 baada ya kutandikwa bila huruma na
wakata miwa Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
Magoli ya Mtibwa Sugar yamefungwa na wachezaji Dickson Daud dakika ya 12, na Hussein Javu dakika ya 43 na 76
Post a Comment