Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu CUF Salim Bimani akifafanua jambo kupitia Katiba katika
mkutano wake wa kupinga matumizi mabaya ya Operesheni inayofanywa na Jeshi la
Polisi na Vikosi vya SMZ kuwatafuta wavunjifu wa amani.Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar
Chama cha Wananchi CUF
kimeliomba Jeshi la Polisi ZanzĂbar kutumia mbinu za kitaalamu katika kuwasaka
na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya uvunjifu wa amani katika
ghasia zilizotokea karibuni ambazo pia zilisababisha kuuliwa kwa Koplo wa Polisi
Said Abdulrahman.
CUF kimelishauri Jeshi
hilo pamoja na Vikosi vya SMZ kuacha kuvamia makazi ya wananchi, na kuwaadhibu
kwa vipigo kwa madai ya kutekeleza Operesheni ya kuwatafuta wahalifu wa matokeo
hayo.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari Ofisini kwake Vuga,Mkurugenzi wa Haki za Binadamu CUF Salim Bimani
amesema Operesheni ya kutumia uvamizi bila kutumia njia za kitaalamu za kutafuta
wahalifu zinakuza mgogoro uliopo badala ya kuupunguza.
Amesema matendo ya
uvunjifu wa Amani na kuuliwa kwa Koplo Said Abdulrahman yanafanana na matukio ya
uvunjifu wa amani Tanzani Bara lakini Jeshi la Polisi Bara limekuwa likitumia
njia za kitaalamu katika kuwakamata wahalifu bila raia wengine wasio na makosa
kuathirika na Operesheni hiyo.
Ametoa mfano wa kuuliwa
kwa Kamanda wa Polisi Mwanza Liberatus Barlow na matukio ya uvunjifu wa amani
Dar es Salaam ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vikosi vya ulinzi
viliweza kutuliza hali hiyo na kufanikiwa kuwakamata wahusika na kupelekwa
mahakani bila hata kuwaathiri wanachi ambao hawakuhusika na kadhia
hiyo.
Ameongeza kuwa Mahala
popote panapohitajika kufanywa Operesheni ya kuwasaka wahalifu mamlaka husika
ndizo zinazobeba dhamana na jukumu la kutumia uataalamu,mafunzo na mbinu
zinazoepusha ukiukwaji wa haki za binadamu na hatimaye kufanikisha
lengo.
Bimani ameongeza kuwa CUF
inalaani kwa nguvu zote vitendo vya fujo na uvunjifu wa amani vilivyofanyika
Octoba 17 hadi 19 vikijumuisha mauaji ya Koplo Said, Salim Hassan Mahaju na
Hamadi Ali Kaimu ambao wote waliuawa kutokana na fujo
hizo.
Kwa upande wao baadhi ya
wananchi ambao waliathirika na fujo hizo wameiomba Serikali kuingilia kati
operesheni hiyo na kutaka kutafutwe njia stahiki za kuwakamata wahalifu bila ya
kuwapiga au kuwanyanyasa ambao hawahusika na fujo
hizo.
Wamedai kuwa tokea
kuanzishwa kwa Operesheni hiyo wamekuwa hawana muda wa kujishughulisha na kazi
zao za kutafuta riziki badala yake wamekuwa wakijifungia nyumbani mwao ili
kujinusuru na vipigo.
Katika
maeneo ambayo Operesheni hiyo imekuwa ikifanywa mara kwa mara ni Bububu,
Amani, Magogoni,
Daraja bovu, Mwanakwerekwe,Mtoni,Kinuni,Mboriborini,Mikunguni
na Kwarara.
Post a Comment