Mheshimiwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib
Bilal amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano maalum wa
wakuu wa nchi za Maziwa Makuu mjini Kampala Uganda leo Oktoba 08, 2012.
Mkutano huu maalum una agenda moja kubwa ambayo ni kujadili na kisha
kupitisha maamuzi kuhusu mustakhbali wa hali ya usalama wa kudumu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.
Mheshimiwa Makamu wa Rais na
ujumbe wake umewasili nchini hapa salama na moja kwa moja kushiriki
kupata taarifa za mikutano ya ngazi ya Mawaziri ambapo Tanzania
iliwakilishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa
Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Omari Juma Mahadhi. Katika mazungumzo hayo ya awali,
Mheshimiwa Waziri Vuai alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa,
Tanzania inabakia kuwa na sifa yake ya siku zote ya kuthamini na kujitoa
kusaidia kupatikana kwa amani katika nchi zinazoizunguka sambamba na
zile zinazohitaji msaada wake. Akifafanua kuhusu makubaliano katika
ngazi ya Mawaziri, Waziri Vuai alimhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais
kuwa Tanzania imewakilishwa vizuri na kwamba nchi nyingine wanachama
zinategemea sana mchango wa Tanzania katika kuisaidia Congo (DRC)
kufikia amani ya kudumu na hivyo wananchi wake kuendelea na shughuli za
kunyanyua vipato vyao bila hofu ya usalama wa maisha yao.
Kwa upande wake Mheshimiwa Naibu
Waziri Mahadhi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu ushiriki wa
Tanzania katika nchi za Maziwa Makuu na akafafanua kuwa nchi hizi
zinategemeana sana katika hali mbalimbali za maisha hivyo Tanzania bado
inayo fursa nzuri ya kuendeleza mahusiano na nchi hizi kwa angalizo
kubwa la kutazama fursa za kiuchumi.
Katika mkutano wa leo wa wakuu wa
nchi uliofanyika katika eneo la Munyonyo nje kidogo ya jiji la Kampala,
Wakuu na Wawakilishi wa wa nchi mbalimbali, walikutana majira ya saa
tano na kisha mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Yoweri Kaguta Museveni
kuufungua. Rais Museveni alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru viongozi wote
akianza na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye alimpongeza kutokana na
ushiriki wake katika mazungumzo ya kufanikisha amani Congo (DRC) na
kisha akamshukuru Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC) kwa kukubali
kuzieleza nchi wanachama wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu hali mbaya ya
kiusalama nchini kwake na kukubali kutaka msaada kutoka kwa nchi hizi.
Mjadala mkubwa katika mkutano huu
ulikuwa kuhusu kuundwa kwa jeshi lisilofungamana na upande wowote ili
lisaidie kumaliza mapigano katika Congo (DRC) na kisha kuiwekea nchi
hiyo misingi ya kuwa na amani ya kudumu. Mkutano huu pia ulihudhuriwa na
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ambaye alikuja na hoja ya kutaka nchi
yake iharakishiwe nafasi ya uanachama katika umoja huu, jambo ambalo
baadhi ya nchi limeona ni bora, lakini zikatoa angalizo kuwa lazima nchi
hiyo licha ya kuwa na nia na sifa ya kuwa mwanachama, ifuate utaratibu
wa kawaida wa kutafuta nafasi ya uanachama na sio kuruka taratibu.
Mkutano huu unafanyika nchini
Uganda wakati nchi hii ikijitayarisha kuadhimisha sherehe za miaka 50 ya
uhuru wake, huku hali vya usalama nchini hapa vikionesha kila sababu ya
kulinda amani katika tukio hili nyeti katika historia ya Uganda na
Afrika Mashariki.
IMETOLEWA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS ,
KAMPALA, UGANDA: OKTOBA 08, 2012
Post a Comment