Na Bin
Zubeiry
SIMBA SC
imetoa sare ya pili mfululizo katika Ligi Kuu hya Vodacom Tanzania Bara, baada
ya kutoka 2-2 na Kagera Sugar jioni hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Kwa matokeo
hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, kutokana na
Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine
mjini Mbeya.
Hadi
mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na
mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya nane,
akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kutoka wingi ya
kulia.
Kwa ujumla
kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa ni Simba
walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’
zaidi.
Kipindi cha
pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa
aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali lililowababatiza mabeki wa timu
hiyo na kutinga nyavuni.
Hilo
lilikuwa bao la tatu kwa Ngassa tangu ajiunge na Simba katika mechi tisa
alizoichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Baada ya
hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia lango la Simba kupitia pembeni
na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa kichwa krosi ya George
Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
Bao
liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya kulishambulia lango la Simba na
katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na
Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja, akiisawazishia
Kagera.
Baada ya
hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira ulinoga zaidi kutokana na
mashambulizi ya pande zote mbili.
Katika mechi
nyingine, Mgambo imeshinda mechi ya tatu mfululizo, baada ya kuifunga Toto
African 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. JKT Ruvu imezinduka baada ya
kuifunga Polisi Morogoro 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na JKT Oljoro
imetoka 0-0 na African Lyon.
Simba SC; Juma Kaseja (Nahodha), Nassor Masoud ‘Chollo’/Uhuru
Suleiman, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto/Edward
Christopher, Amri Kiemba, Haruna Moshi/Jonas Mkude, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi
na Mrisho Ngassa.
Kagera Sugar; Andrew Ntala, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus
Nesta (Nahodha), Benjamin Effe/Themi Felix, Malegesi Mwangwa, Daudi
Jumanne/Kamana Salum, George Kavilla, Shijja Mkinna, Enyinna Darlington na
Wilfred Ammeh/Paul Nwai.
Katika
mchezo wa awali, Simba B iliifunga Moro United mabao 3-0 katika mchezo wa
utangulizi kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na
Kagera Sugar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya
Simba B inayofundishwa na Suleiman Matola, akisaidiwa na Amri Said ‘Stam’
yalipatikana yote kipindi cha pili, wafungaji Ramadhan Salum dakika ya 65 na 70
na Miraj Athumani dakika ya 85. Moro United inajiandaa na Ligi Daraja la
Kwanza, inayotarajiwa kuanza Oktoba 24, mwaka huu
Post a Comment