Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

IWEJE UMLAZIMISHE MTU USIYE NA MAPENZI NAYE?


MAMBO vipi watu wangu? Natumaini kwamba mambo ni freshi na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi ni mzima bukheri wa afya na tunakutana tena kupitia safu hii lengo likiwa ni lile lile la kuwekana sawa katika masuala kadhaa yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita niliandika mada iliyokuwa inaeleza jinsi wapenzi wanavyoweza kujifunza kutokana na kifo cha msanii maarufu, Steven Kanumba. Ni matumaini yangu mmejifunza kitu na kubadilika itakuwa ni jambo jema kwenu.
Baada ya utangulizi huo, nigeukie sasa kwenye mada yangu ya wiki hii. Wakati flani huwa najiuliza kwa nini tunakuwa na wapenzi, kwa nini mapenzi yakawepo? Kwa nini tunaoa ama kuolewa? Kwa nini baadhi ya watu huamua kujinyonga baada ya kuachwa na wapenzi wao? Kwa nini mapenzi yamekuwa sehemu ya maisha yetu?
Kwa nini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Huwa najiuliza maswali mengi na kupata majibu mengi pia.
Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mapenzi hayo hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Elewa kwamba kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi. Kama ndivyo, kwa nini ukubaliane na hali hiyo ambayo unaweza kuepukana nayo?
Unadhani hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana! Huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye unaona wazi kwamba hampendi.
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi maisha yako yatakuwa yenye furaha isiyosimulika. Mapenzi yapo hivyo na kama ukienda kinyume chake lazima utaumia.
Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake na hao hao ndiyo wamekuwa wakiongoza kwa kutoa machozi pale wanapotendwa.
Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye. Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria. Mapenzi hayafikiriwi kiivyo ndugu zangu.
Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako utakuambia bila kukuficha na utabaki wewe tu kufanya maamuzi sahihi. Hii ina maana kuwa atakapokuambia anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana na lazima utamkaribisha.

Tatizo lilipo
Baadhi ya wasichana wakitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubalia kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo kitu ambacho hakipo katika ulimwengu wa mapenzi.
“Fedha anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitakwenda naye hivyo hivyo mwisho wa siku penzi litajijenga lenyewe taratibu,” baadhi ya wasichana huwaza hivyo. Baada ya wazo hilo kuingia akilini mwake, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa.
Madhara yake
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati ambalo ndiyo msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote. Kinyume cha hivyo, furaha utakuwa ukiisikia kwenye bomba tu.
Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati. Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo na kama ana hasira, anaweza kukuua.
JAMBO LA MSINGI
Ushauri kwangu ni kwamba, kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu wa watu wanaoingia kwenye uhusiano na watu ambao hawajawapenda.
Maisha yenyewe ni mafupi hivyo kuwa makini, fanya maamuzi sahihi yahusuyo maisha yako ya kimapenzi kwa umakini wa hali ya juu ili usije ukawa mmoja kati ya wanaolizwa na mapenzi na kuishia kujuta kila siku.
 
Chanzo: UjanaTz
 
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top