Naibu Waziri wa Chakula na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, jana wamezindua shindano la Maisha Plus/Mama Shujaa wa Chakula 2012.
Uzinduzi
huo umeshuhudia wanawake 14 waliongia kambini kwenye kijiji cha Maisha
Plus ambao baadaye wataungana na vijana watakaoshiriki kwenye shindano
la Maisha Plus.
Akizungumza
baada ya kuwatambulisha Mama Shujaa 14 watakaoshiriki kwenye shindano
hilo kumpata mshindi mmoja, Mheshimiwa Malima alisema serikali
itahakikisha kuwa mwanamke ambaye ni mzalishaji mkuu wa chakula kwenye
jamii ya Tanzania anawekewa mazingira mazuri ambayo yatasaidia shughuli
za kilimo ziwe na tija zaidi.
Kwa
upande wake Mheshimiwa Mwalimu alisema wanawake wamekuwa wakikumbwa na
changamoto nyingi kwenye jamii ambapo pamoja na kushiriki katika
uzalishaji wa chakula wamekua wakikosa mamlaka na uamuzi wa kile
wanachokitayarisha kutokana na kuendelea kuwepo kwa mfumo dume ambapo
mwanaume huwa juu ya mwanamke.
Alisema
wanatambua kuwa kipato kinachopatikana kutokana na shughuli za kilimo
kinamilikiwa na wanaume ambapo pia wanawake wengi hawamiliki ardhi.
Aliongeza kuwa serikali inazitambua changamoto hizo na inafanya kazi kuziondoa kabisa.
Mheshimiwa
Mwalimu alisisitiza kuwa shindano la Mama Shujaa lengo lake ni
kuikumbusha jamii umuhimu wa mwanamke katika uzalishaji wa chakula na
kwamba sheria inasema mwanamke na mwanaume wana haki ya sawa katika
maamuzi ya kile wanachozalisha.
Naye
Mkurugenzi mkazi wa shirika la OXFAM ambalo ni wadhamini wa shindano
hilo Bi. Monica Gorman alisema wanawake ni waendeshaji wa uchumi wa
Tanzania lakini umuhimu wao umefunikwa kwa muda mrefu hivyo kwa kutumia
shindano la Mama Shujaa wa Chakula, wanawake wanamulikwa ili wapate kile
wanachostahili.
Shindano
hilo lina lengo la kuwainua wanawake, kuwapa moyo na kuwaunga mkono
wakulima wadogo wanawake nchini na kuongeza kukubalika kwa mchango wao
katika kilimo.
Uzinduzi wa Maisha Plus/Mama Shujaa wa Chakula 2012 ulioneshwa live kupitia kituo cha TBC1.
on Wednesday, October 3, 2012
Post a Comment