MGOMBEA
udiwani kata ya Daraja Mbili kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo, (CHADEMA), Prosper Msofe, amelazwa kwenye hospitali ya mkoa
ya Mount Meru akisumbuliwa na maumivu ya uti wa mgongo baada ya
kuzuiliwa kwenye kituo cha polisi cha kati, Arusha usiku wa juzi kuamkia
jana.
Katibu wa
wilaya ya Arusha wa CHADEMA, Martin Sarungi, na aliyekuwa mbunge wa
Arusha, Godbless Lema, waliwaeleza waandishi wa habari mbele ya kituo
cha polisi kuwa mgombea wao alikamatwa majira ya saa mbili usiku eneo la
Friends Corner baada ya kuhoji sababu wamachinga kunyang’anywa bidhaa
zao na Ramadhan Kalamba (56) anayedai kuwa halmashauri ya jiji imempa
jukumu la kuwaondoa machinga katikati ya jiji.
“Msofe
alihoji sababu za Ramadhan kuchukua mali za wamachinga majira ya usiku
wakati ambao halmashauri haifanyi kazi; alikuwa akizipeleka wapi na ni
nani aliyempa mamlaka ya kuchukua vitu hivyo ndipo gari la polisi
likafika na kumchukua,” alisema Lema.
Walisema
kuwa baada ya kupata taarifa za mgombea wao huyo kukamatwa, baadhi ya
wanachama na viongozi walimfuatilia mpaka kituo cha polisi kwa lengo la
kumwekea dhamana jambo ambalo lilishindikana ndipo majira ya saa nne
usiku wakaamua kuondoka.
Hata hivyo
Kamanda wa Polisi mkoani hapa (RPC), Liberatus Sabas, alikanusha madai
hayo kwa kile alichoeleza kuwa mgombea huyo hakunyimwa bali alikataa
dhamana mwenyewe ambapo alidai kuwa alikamatwa na askari wa doria na
kufikishwa polisi kwa tuhuma za kumpiga ngumi ya kifuani Kalamba.
Alisema kuwa
jeshi la polisi lilipata taarifa kuwa Kalamba anashambuliwa ndipo
askari wa doria walipofika na kumchukua Msofe ambapo alisema kuwa mzozo
baina ya wawili hao ulitokana na hatua ya Msofe kuhoji sababu za Kalamba
kutaka wamichinga hao waondoke eneo hilo huku akijaribu kumzuia
asiendelee kutangaza.
Awali jana
majira ya saa nne asubuhi mgombea huyo wa CHADEMA alienda kupatiwa
matibabu kwenye zahanati ya polisi akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi
la polisi ambapo daktari wa zahanati hiyo alishauri apelekwe hospitali
ya mkoa kwa uchunguzi zaidi lakini polisi waliamua kumpeleka mahakama ya
mwanzo ya Maromboso.
Baadhi ya
viongozi wa CHADEMA waliokuwa mahakamani hapo walikwenda kuuona uongozi
wa mahakama na kuwaonyesha cheti alichopatiwa mtuhumiwa huyo
kinachomtaka apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi jambo ambalo
linadaiwa pengine ndilo lililopelekea mtuhumiwa huyo kutofikishwa mbele
ya hakimu.
Mgombea huyo
ambaye alikuwa amepakiwa kwenye gari ya polisi yenye namba za usajili
PT 1844 ambayo ubavuni imeandikwa OCD Arusha alikaa rumande ya mahakama
hiyo kwa zaidi ya saa moja ambapo gari hilo lilirudi likiwa limeongeza
idadi ya askari wenye silaha wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hii
(OCD), G. A Muroto na kumchukua ambapo walimpeleka moja kwa moja
hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Wagombea
wengine katika kinyang’anyiro hicho na vyama vyao kwenye mabano ni
Philip Philip (CCM), Mohamed Msuya (NCCR-Mageuzi), William Laizer (TLP)
na Zani Zakaria (CUF).
chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment