RAIS Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi jana alipanda
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutoa
ushahidi katika kesi ya kuibiwa zaidi ya Sh37milioni.Mwinyi anakuwa Rais
mstaafu wa pili kupanda kizimbani katika historia ya Tanzania baada ya
Mei 7, mwaka huu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kupanda
kizimbani mahakamani hapo kutoa ushahidi katika kesi ya aliyekuwa Balozi
wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.
Katika kesi
hiyo, Profesa Mahalu alikuwa anakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi.
Hata hivyo, Mahakama ilimwachia huru baada ya kumwona hana hatia.Mzee
Mwinyi alipanda kizimbani katika kesi namba 201 ya mwaka huu
inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, Geni Dudu kutoa ushahidi wa kuibiwa
kiasi hicho cha fedha mtuhumiwa akiwa ni wakala wake, Abdallah Nassoro
Mzombe (39) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni Mkwajuni,
Dar es Salaam.
Mzombe anadaiwa kumwibia Rais Mstaafu Mwinyi jumla ya Sh37,440,000 zikiwa ni kodi ya pango katika nyumba mbili anazomiliki.
Kabla
ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, Rais Mwinyi aliingizwa chemba namba
moja kwa ajili ya kuandaliwa na Wakili wa Serikali, Charles Anindo na
wakati huo maofisa wanne wanaodaiwa kuwa ni wa Usalama wa Taifa
wakizunguka nje ya mlango wa ofisi hiyo ya Mahakama.
Ilipofika saa
5:05 asubuhi, askari mmoja wa Magereza alimpandisha mshtakiwa huyo,
Mzombe mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yake.
Baada
ya mshtakiwa huyo kupandishwa na waandishi wa habari wote waliokuwepo
kwenye eneo hilo nao wakijiandaa kuingia mahakamani ili kusikiliza kesi
hiyo, maofisa hao waliwazuia.
Kati ya maofisa hao wanne, mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika aliwahoji waandishi kabla ya kuwazuia kuingia:
Swali: Mnakwenda wapi?
Jibu: Tunakwenda mahakamani.
Swali: Nyie ni akina nani?
Jibu: Waandishi wa habari
Swali: Mmeambiwa kuna mahakama humu?
Jibu: Ndiyo hiyo ni mahakama.
Baada
ya waandishi wa habari kujibu hivyo, ofisa huyo aliwazuia kuingia
kwenye Mahakama hiyo akisema... “Msiingie huku hii haiwahusu.”
Baada
ya kuambiwa hivyo waandishi wa habari walikaa nje hadi saa 6:21 Rais
Mwinyi alipomaliza kutoa ushahidi wake na kuondoka mahakamani hapo.
Kwa
mujibu wa kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza
Agosti 21 mwaka huu, Mzombe anadaiwa kufanya makosa hayo kinyume na
Kifungu cha 258 na 273 (b) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya
16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ilidaiwa kuwa kati ya
Januari Mosi, 2011 na Julai 2012, huko Mikocheni, Mzombe akiwa Wakala wa
Rais huyo mstaafu, alimwibia Sh17,640,000 ambazo ni pato la kodi ya
nyumba yake iliyopo eneo la Mikocheni Wilaya ya Kinondoni.
Iliendelea
kudai kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho Mzombe alimwibia Rais Mwinyi
kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba namba 481, iliyopo kwenye Kiwanja A
huko Mikocheni ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Mbali na shtaka
hilo, pia anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2011 na Julai 10, mwaka
huu huko Msasani Village Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa huyo alimwibia
tena Rais huyo mstaafu Sh19,800,000 ambazo zilikuwa ni kodi ya nyumba.
Iliongezwa kudaiwa kuwa kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba hiyo la mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
chanzo: Tanzania Daima
Loading...
Post a Comment