
Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa,David Shambwe (wa pili kulia) akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa kuzindua rasmi mauzo
ya nyumba katika mradi wake mpya wa Mindu,Upanga jijini Dar es Salaam.Wengine
pichani toka kulia ni Meneja Mahusiano ya Jamii wa Shirika la Nyumba la
Taifa,Muungano Saguya,Meneja Masoko na Utafiti wa Shirika la Nyumba la
Taifa,Itandula Gambalagi na mwisho ni Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa
wa Upanga,Benedict Kilimba.


Meneja Masoko na Utafiti wa
Shirika la Nyumba la Taifa,Itandula Gambalagi akiwaonyesha baadhi ya Waandishi
wa Habari sehemu ya Mradi wa Jengo Jipya lililopo Mtaa wa Mindu,Upanga jijini
Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa,David Shambwe akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kutembelea mradi wake mpya wa
Mindu,Upanga jijini Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine tena
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) leo 24 Oktoba, 2012 limezindua rasmi mauzo ya
nyumba katika mradi wake mpya wa Mindu, jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa mradi huu ulianza
rasmi mwezi Novemba mwaka 2011, na unatarajiwa kukamilika rasmi Aprili 2013 na
mteja kuweza kukabidhiwa nyumba yake mwezi Mei 2013, ikiwa ni miezi 18 baada ya
kuanza ujenzi. Mradi unatarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni
11 mpaka utakapomalizika, fedha zinazogharamiwa na Shirika kutoka vyanzo
mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha za mikopo ya benki.
Mradi huu uliopo mtaa wa
Mindu eneo la Upanga, takribani mita 100 kutoka Hospitali Kuu ya Taifa
Muhimbili, una sehemu ya nyumba 60 za kuuzwa zilizopo kwenye majengo pacha ya
ghorofa 15, uko sehemu zenye huduma zote muhimu za kijamii zikiwamo hospitali,
shule, maduka, na masoko. Pia Mradi unatarajiwa kuboresha maisha ya wanunuzi wa
nyumba hizi kwani upo karibu kabisa na katikati ya jiji na kwamba mnunuzi
anaweza kwenda kazini bila kutumia gharama yoyote ya usafiri wa
gari.
Aidha, nyumba zipo ndani ya
uzio kwa ajili ya usalama wa wakaazi wake na kuna maegesho ya magari ya kutosha.
Nyumba 60 tu zinazouzwa ambapo kila nyumba ina vyumba vitatu vya kulala, vyo
vinajitegemea. Kila nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 141 (sq.m), sebule
iliyoungana na eneo la kula chakula, choo cha umma, jiko kubwa la kisasa na eneo
la kufulia na kuanikia nguo.
Sifa za ziada za mradi huu
ni kuwa na eneo maalum la kukusanyia taka, nyumba zote zina viyoyozi, vifaa vya
kung’amua moto, sehemu iliyotengwa maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi (gym),
bwawa la kuogelea (swimming pool) na eneo kubwa la ziada la maegesho ya
magari.
Kila nyumba itauzwa kwa
bei ya TZS 272,050,673.08 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT ) na TZS
321,019,794.24 ikiwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT). Tunawahamasisha na
kuwakaribisha watanzania wote walio nchini na nje ya nchi kujitokeza ili kununua
nyumba hizo.
Wanaweza kufanya
mawasiliano na Makao Makuu ya Shirika, Ofisi zetu za Mikoa au kupitia barua pepe
na kukamilisha taratibu mapema kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mchakato ulio
wazi wa manunuzi. Katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba, Shirika
linajenga nyumba za gharama ya juu, kati na chini ili kuwahudumia watanzania wa
kada zote.
Katika azma hiyo, nyumba
10,000 zitakazojengwa kufikia 2015 zitahusu watu wa kipato cha juu na nyumba
5,000 zitakazojengwa kufikia mwaka huo zitakuwa ni nyumba za watu wa kipato cha
chini.
Shirika limeanza kujenga
nyumba za gharama ya kati na juu ili kupata faida itakayoliwezesha kuwajengea
watu wa kipato cha chini nyumba za gharama nafuu. Hii inatokana na ukweli kuwa
Shirika halipati ruzuku toka serikalini ya kujenga nyumba kwa ajili ya wananchi
wa kipato cha chini.
Mradi huu wa Mindu
tunaouzindua hii leo, ni moja ya miradi ya ujenzi wa nyumba za watu wenye kipato
cha juu.. Ukiwa mdau na mnunuzi mtarajiwa, ama una ndugu/rafiki anayetamani
kununua nyumba katika mradi huu, wasiliana na Kitengo cha Mauzo simu namba 0754
444 333; barua pepe: sales@nhctz.com na pia tembelea tovuti ya Shirika
www.nhctz.com kwa maelezo zaidi.


Post a Comment