Wachezaji wa Simba kwa raha zao |
SIMBA SC
imezinduka kutoka kwenye wimbi la sare katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
baada ya kufanikiwa kuichapa Azam FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Ushindi huo,
unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22,
baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC inapromoka hadi nafasi ya tatu kwa
pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa, ikiipisha Yanga nafasi ya pili,
ambayo imetimiza pointi 20 baada ya kuifunga JKT Oljoro
leo.
Mabao ya
Simba leo yalitiwa kimiani na Emanuel Arnold Okwi mawili na Felix Mumba Sunzu
Jr. moja, wakati la Azam lilifungwa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
Hadi
mapumziko, tayari Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1, Azam wakitangulia kufunga
dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng
na kumchambua Juma Kaseja.
Dakika mbili
baadaye, Sunzu aliisawazishia Simba, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya
Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa
Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto.
Kipindi cha
pili Simba walirudi na moto wao na iliwachukua dakika tano tu kuhitimisha karamu
yao ya mabao, baada ya Okwi kuwainua tena vitini mashabiki wa Simba, akifumua
shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa
Azam.
Mrisho
Ngassa ndiye alikuwa nyota wa mchezo wa leo, kutokana na kuisumbua mno Azam,
iliyomuuza kwa mkopo Simba miezi miwili
iliyopita.
Simba SC;
Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Shomary
Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Ramadhan Chombo, Mwinyi Kazimoto, Felix
Sunzu/Ramadhan Singano, Mrisho Ngassa/Christopher Edward na Emmanuel
Okwi.
Azam FC;
Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad na Aggrey Morris,
Abdulhalim Humud, Jabir Aziz/Abdi Kassim, Himid Mao/Kipre Balou, John Bocco
‘Adebayor’/Khamis Mcha, Kipre Herman na Salum
Abubakar.
Katika
mchezo uliotangulia, Azam B iliifunga Simba B 1-0, bao pekee la Kevin Friday
dakika ya 56.
Kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga iliibuka na ushindi wa 1-0, bao
pekee la beki Mbuyu Twite, hilo likiwa bao lake la tatu tangu ajiunge na timu
hiyo kwenye ligi hiyo.
Kwa ushindi
huo, Yanga imetimiza pointi 20, baada ya kucheza mechi 10 na kupanda nafasi ya
pili.
Mechi
nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya African Lyon imetoka sare ya 1-1 Kagera
Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Polisi
Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
Mechi kati
ya Mgambo JKT na Prisons iliyokuwa ichezawe leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
imeahirshwa kutokana na wachezaji wa Prisons kupata ajali wakiwa njiani kuelekea
Tanga.
Ligi hiyo
itaendelea kesho kwa michezo miwili kati ya JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM
Kirumba, Mwanza.
chanzo: Bin zubeiry
Post a Comment