TAHADHARI YA UGONJWA WA
MARBURG
Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO), tarehe 20 Oktoba, 2012 kuhusu ugonjwa wa Marburg ambao umejitokeza katika
nchi jirani ya Uganda. Maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo ni Wilaya ya Kabale,
Kanda ya Kusini Magharibi ya nchi, na wilaya hii inapakana na Rwanda. Mpaka
tarehe 24 Oktoba 2012, takriban watu 13 wamepata maambukizo na 6 wamepoteza
maisha..
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda
kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania
na hasa wale waliopo katika mikoa ambayo inapakana na na nchi jirani ya Uganda
(Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Kigoma).
Marburg
ni ugonjwa wa hatari unaofanana na Ebola na unasababishwa na virusi
vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalam “Marburg Virus”. Ugonjwa huu ni miongoni mwa
magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za Virusi zinazosababisha kutokwa
damu mwilini, (Viral Haemorrhagic Fevers). Chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa
huu hakijulikani. Hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Ugonjwa huu
hauna tiba wala chanjo.
Dalili kuu za ugonjwa huu ni pamoja na Homa kali, inayoambatana na kutokwa damu
katika matundu yote ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni,
masikioni, machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda
mfupi.
Kipindi cha kuonekana kwa dalili za
ugonjwa ni kati ya siku 3 hadi 9 baada ya kupata
maambukizi.
Ugonjwa huu unaenea kwa urahisi sana na
haraka kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa na
kugusana na mate, damu, mkojo, machozi, kamasi, maji maji mengine ya mwili,
ikiwa ni pamoja na jasho au kumgusa mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa
Marburg.Ugonjwa huu pia unaweza kuenezwa iwapo mtu atagusa nguo au mashuka ya
mgonjwa wa Marburg.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua
hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa
huu:
- Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya. Aidha taarifa hii pia imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet” ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli na vipeperushi vinavyoelezea ugonjwa huu.
- Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipaka. Aidha watalaamu hawa wa Afya pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huu ili endapo ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
- Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyeripotiwa nchini. Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha
huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote
atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Kitengo cha mawasiliano ya
Serikali
25/10/2012
Post a Comment