Rais wa TFF, Tenga akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Kulia ni Sunday Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na kushoto, Katibu, Angetile Osiah |
Na Mahmoud
Zubeiry
RAIS wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba timu ya
taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inahitaji zaidi ya Sh
Milioni 225 kwa ajili ya kampeni yake iliyobakia ya kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari makao makuu ya TFF, Ilala, Dar es Salaam, Tenga alisema
kwamba shirikisho lake kwa sasa halina fedha hizo, kwa sababu hiyo haina
mdhamini, zaidi ya kutegemea misaada ya wadau.
Tenga
alisema tayari Kamati ya Vijana ya TFF imekwishakutana kuweka mikakati ya
kuiwezesha Serengti kushiriki vema kampeni hizo, ikiwemo kuunda Kamati ya
kuisaidia timu hiyo.
Hata hivyo,
Tenga hakuitaja Kamati iliyoundwa kwa sababu bado hawajazungumza na Wajumbe
walioteuliwa.
Alisema
kocha wa timu hiyo, Mdenmark Jacob Michelsen ameomba mechi za kujipima nguvu
kabla ya kucheza na Kongo Brazaville kuwania tiketi ya Morocco na Kamati ya
Vijana inahangaikia suala hilo kwa sasa.
Alisema
tayari kuna mwaliko kutoka Botswana wa Serengeti kwenda kucheza, lakini kutokana
na ukosefu wa fedha wanashindwa hadi sasa kutoa
jibu.
Kikosi cha
wachezaji 25 cha Serengeti Boys kipo kambini mjini Dar es Salaam tangu Oktoba
21, mwaka huu kujiandaa na mechi hiyo, ya kwanza ikichezwa nyumbani Novemba 17,
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili
baadaye.
Tanzania
imefuzu bila jasho hadi kufika hatua hiyo, baada ya wapinzani wake wa awali,
Kenya na Misri kujitoa katika Raundi ya Kwanza na ya
Pili.
Kama
Tanzania itafuzu kushiriki Fainali hizo za mwakani, itapoza machungu ya mwaka
2005 walipofuzu kucheza Fainali za Vijana wa umri huo kwa kuzitoa Rwanda, Zambia
na Zimbabwe, lakini baadaye kwa sababu ya ‘kufoji’ umri wa Nurdin Bakari,
ikaondolewa mashindanoni.
Zaidi ya
Fainali za Mataifa ya Afrika 1980 na CHAN 2009, katika soka ya wanaume, Tanzania
haijashiriki fainali nyingine zozote za Afrika tangu iingie kwenye soka ya
kimataifa.
Post a Comment