UMOJA wa Ulaya unafanya
mchakato wa kuanzisha jeshi la kuaminika nchini Mali, ambako waasi wenye itikadi
kali ya Kiislamu wamelidhibiti eneo la kaskazini baada ya mapinduzi ya kijeshi
nchini humo.
Hayo ni kwa mujibu wa
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Mauel Barroso, aliyezungumza
akiwa pamoja na Rais Thomas Boni Yayi wa Benin, katika mkutano na waandishi
habari kwa mara ya kwanza tangu kuwepo madai ya kupanga njama ya kumuua kwa
kumpa dawa yenye sumu.
Barroso ambaye alikuwa
Cote d'Ivoire, amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaendelea kuwa makini sana
na hali nchini Mali. Ameongeza kusema kuwa kwa sasa wanafanyia kazi mipango
kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kuna serikali na jeshi la
kuaminika nchini Mali.
Rais wa halmashauri ya
umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso,(kulia) akiwa na kansela
Merkel.
Makundi yenye itikadi
kali wakiwemo wanachama wa tawi la mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda kaskazini mwa
Afrika, wamelitwaa eneo la kaskazini la Mali huku kukiwa na machafuko
yaliyotokana na mapinduzi ya kijeshi mwezi Machi mwaka huu, ambayo yalifanywa na
wanajeshi wa vyeo vya chini.
Serikali
yashindwa
Hata hivyo, serikali ya
mpito ya kiraia imeshindwa kujizatiti na serikali za mataifa ya Magharibi
zinahofia kuwa eneo hilo linaweza kuwa makaazi ya wapiganaji wenye itikadi
kali.
Rais wa Benin Thomas
Boni Yayi.
Viongozi wa Ulaya
wameahidi kukiunga mkono kikosi cha jeshi cha Afrika ambacho kitapelekwa Mali
kuwaondoa waasi hao, lakini wamesema msaada wao hautahusisha kupelekwa kwa
wanajeshi wa Umoja wa Ulaya.
ECOWAS pia yataka
kusaidia
Jumuiya ya Kiuchumi ya
Afrika Magharibi-ECOWAS, ambayo Benin ni mwanachama, imesema iko tayari kupeleka
kikosi cha kijeshi nchini Mali, lakini sababu kadhaa zinachelewesha mpango wa
kupelekwa kwa kikosi hicho.
Mkutano wa ECOWAS
kuijadili Mali mjini Yamoussoukro.
Rais Yayi ambaye kwa
sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, amesema yeye na Barroso wamejadiliana
kuhusu jukumu la Ulaya kwenye mzozo wa Mali, lakini hakuzungumzia chochote
kuhusu njama za kutaka kumuua.
Kwa mujibu wa waendesha
mashtaka, mpwa wa Rais Yayi, daktari wake na wengine walipanga njama za kumuua
kwa kumpa dawa za kutuliza maumivu zenye sumu.
Watu watatu wanaripotiwa
kushikiliwa, huku vibali vya kuwakamata watuhumiwa wengine wawili vikiwa
vimetolewa.
Baadhi ya watu
wanaasema kuwa madai hayo yalikuwa na lengo la kuwachafua maadui wa rais,
akiwemo mtuhumiwa kinara wa kupanga njama hizo, mfanyabiashara Patrice Talon,
ambaye alikuwa akimuunga mkono Rais Yayi kabla ya kuripotiwa kuhitalifiana na
rais huyo kutokana na mzozo wa mikataba.
Post a Comment