Rais Kikwete akizindua rasmi mradi mkubwa wa
kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania jijini Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Novemba Mosi, 2012, amezindua rasmi mradi
mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania unaojulikana kama Mradi wa
Uboreshaji Miji ya Tanzania (Tanzania Strategic Cities project – TSCP)
utakaogharimu mabilioni ya fedha.
Aidha, Rais Kikwete amezidua rasmi Jiji la Arusha
katika sherehe ya kufana iliyofanyika kwenye Mnara wa Azimio la Arusha katikati
ya jiji hilo. Mradi wa TSCP unalenga kuboresha huduma za msingi katika miji saba
na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kujenga upya, kukarabati
na kupanua miundombinu pamoja na kuijengea uwezo wa kukusanya na kusimamia
mapato ya miji husika.
Mradi huo ni mmoja ya miradi mitatu inayogharimiwa
na Benki ya Dunia kwa nia ya kuboresha miji ya Tanzania. Mbali na TSCP, miradi
mingine ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam
Metropolitan Development Project - DMDP) na Urban Local Government Strengthening
Programme (ULGSP). Mpaka sasa Benki hiyo imekwishakutoa sh bilioni 8.76 kati ya
sh bilioni 34.7 za TSCP.
Chini ya TSCP ambao unagharimu kiasi cha sh bilioni
191.3 miji itakayonufaika ni Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya,
Mtwara na CDA ambayo ndiyo itakayopata pesa kubwa zaidi kuliko mjini mingine.
Aidha, chini ya TSCP, miji hiyo itajengewa miundombinu ya barabara zenye jumla
ya kilomita 141.2, ujenzi wa madampo matano, ununuzi wa vifaa vya kusimamia taka
ngumu, vituo vya mabasi sita, vituo viwili vya kuegesha malori na kilomita 15.9
za mitaro ya maji ya mvua. Katika mji wa Arusha, kiasi cha barabara za lami
zenye urefu wa kilomita 7.23 zitajengwa, mtaro mkubwa wa maji ya mvua wa mita
800 utajengwa, zitafungwa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara
tatu ambazo ni Sokoine na Viwandani, Sokoine na Esso na Kanali Middleton na
Makongoro. Katika awamu ya pili, kiasi cha barabara zenye urefu wa kilomita 7.8
zitajengwa katika Jiji la Arusha.
Miji itakayonufaika na ULGSP ambako Benki ya Dunia
inatoa mkopo wa dola za Marekani milioni 255 na unatarajiwa kuanza katika mwaka
ujao wa fedha ni Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea,
Singida, Musoma, Iringa, Bukoba, Lindi, Njombe, babati, Kibaha, Mpanda, Geita,
Korogwe na Bariadi. DMDP kwa ajili ya Jiji la Dar Es Salaam, itahusika wilaya
zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke na utagharimu kiasi cha dola za Marekani
milioni 75.
Baada ya kuzindua mradi huo wa TSCP, Rais Kikwete
amezindua Jiji la Arusha ambalo linapanda hadhi kutoka Manispaa. Katika uzinduzi
huo, Rais amezindua nembo ya Jiji pamoja na kukabidhi cheti cha kulipandisha
hadhi Jiji hilo. Rais Kikwete amezindua miradi hiyo ikiwa ni shughuli zake
katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo katika Mkoa wa Arusha. Rais amewasili Arusha mchana wa leo kutoka
Dodoma.
bango la mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza
miji ya Tanzania
Rais Kikwete akisalimiana na Mbunge wa
Arumeru Mashariki Mhe. Joshua Nassari katika sherehe za
uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya
Tanzania jijini Arusha
Wakaazi wa Arusha wakimshangilia Rais Kikwete
alipowasili katika sherehe za uzinduzi rasmi wa mradi
mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania
Post a Comment