Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesema mpasuko uliopo ndani ya chama hicho unatokana na makundi yanayotaka uongozi wa juu ikiwamo nafasi za urais mwaka 2015.
Aidha, amesema hana kundi lolote analoliunga mkono ndani ya chama hicho na kuwataka wanaotaka aingie katika makundi yao wamwache.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM katika Ukumbi wa Kizota nje kidogo ya Mji wa Dodoma, Rais Kikwete alisema ukiondoa mpasuko unatokana na kuwania madaraka, hali ndani ya chama hicho ni shwari.
“...Chama bado kiko imara, ukiacha makundi hayo ambayo hata mimi wananilazimisha niwe kwa baadhi ya kundi na mimi nikawaambia siwezi kuwa katika kundi moja maana mimi ni mwenyekiti, itakuwaje katika kikao cha uamuzi?” alisema.
Katika hotuba yake iliyochukua saa 1:48, mwenyekiti huyo alisema, anazo taarifa na hata kujionea kwa macho kuwa uamuzi wa baadhi ya wanaCCM kugombea madaraka, ndiyo unaosababisha migogoro ndani ya chama.
“Nikiwauliza kama nani anajua migogoro ndani ya chama chetu kuwa ipo mtajibu nini? Nawahakikishia kuwa inatokana na watu wanaoutaka uongozi ikiwamo kutangaza nia za urais, ubunge na udiwani.”
Alisema robo tatu ya migogoro yote ya ndani ya CCM inatokana na watu kutaka vyeo, lakini akasema kufanya hivyo si dhambi na wala wanaowaunga mkono watu wengine wasihesabiwe kuwa watenda dhambi.
Mwenyekiti huyo alisema watu wanapotangaza ni zao, kumekuwa na malumbano na migongano inayosababisha kutokuelewana jambo alilokemea akisema halifai kuwapo, kwani linaelekea kukimomonyoa chama hicho.
Hata hivyo, aliwataka wanaotangaza nia, kuishia kuonyesha dhamira zao na wasithubutu wala kujaribu kukiua chama akiwatishia kuwa nao hawatabaki salama.
Alisema wenye ndimi mbili hawapaswi kuwapo ndani ya chama akisema watatimuliwa wakatafute maeneo mengine katika vyama vingine ambako wanaamini watapata nafasi.
Aliwataka wapambe wa wagombea kuacha kuendeleza migogoro akijitolea mfano kwamba alikuwa na wapambe wakati anawania urais, lakini wote walibaki kitu kimoja.
chanzo: Mwananchi
Alisema wenye ndimi mbili hawapaswi kuwapo ndani ya chama akisema watatimuliwa wakatafute maeneo mengine katika vyama vingine ambako wanaamini watapata nafasi.
Aliwataka wapambe wa wagombea kuacha kuendeleza migogoro akijitolea mfano kwamba alikuwa na wapambe wakati anawania urais, lakini wote walibaki kitu kimoja.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment