Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Kwanini wanawake wanaamua kubaki na waume wanaosaliti mahusiano ya ndoa?

 




Kwanini watu huingia kwenye ndoa?
Kuna watu watakuambia “najua kuoa, sijui kuacha”. Wengine watakuambia, ndoa ni taasisi ambayo waliomo wanataka kutoka, walio nje wanataka kuingia”. Ukweli ni upi?
Watu huoana kufuatana na utashi wao na sababu wanazozijua wenyewe. Hata hivyo ni sawa tukisema kwamba watu wengi huingia kwenye ndoa kwa lengo la kuishi na yule wampendae kwa kadri
inavyowezekana. Kwa wale ambao viapo vyao vya ndoa vinasema “hadi kifo kiwatenganishe”, tunaweza kusema kwamba, wanaingia kwenye ndoa kwa maisha ya kudumu pamoja hadi watakapoiaga dunia. Ndoa inawapatia wanandoa uhalali kiimani, kimila na kisheria wa kuishi kinyumba, kuzaa na kulea watoto, kutunzana, kupendana kwa kiwango cha juu na pia kuhudumiana. Mwanandoa anapata haki zake na kubanwa kutekeleza wajibu unaompasa kutimiza.Kwa maneno mengine ndoa zina miiko yake na kanuni na taratibu zake ambazo zinapaswa kuzingatiwa ili ndoa isimame.

Pamoja na kwamba lengo la kuoana ni kuishi na kudumu pamoja, hali halisi ni kwamba kuoana na kuachana siku hizi ni jambo la kawaida. Ndoa zinafungwa tena kwa gharama kubwa. Watu wanasherehekea na kushuhudia viapo vya mke na mume kuishi pamoja maisha yao yote tena kwa mapenzi makubwa katika hali zote. Ni ya kweli hayo au ni mchezo wa kuigiza tu? Baada ya sherehe na cherekochereko wanandoa wanaanza maisha katika hali halisi ya maisha. The party is over. Kufumba na kufumbua unasikia hawapo tena pamoja. Sababu zipo nyingi ikiwemo kukosa uvumilivu na subira.
Mwanzo wa ndoa tunaambiwa ni tamu kama chungwa, katikati ni tamu kama limao au ndimu na mwishowe huweza kuwa chungu kama shubiri! Inapokuwa kwenye utamu wa chungwa, wanandoa huwa kwenye ulimwengu wa kivyaovyao, wa kiparadiso fulani na siyo rahisi kufikiria kuna siku ndoa hiyo itakapogeuka kuwa chungu! Maisha ya ndoa, siyo lelemama, ni safari isiyo na ramani inayoeleweka. Kuna sehemu itakuwa tambarare, mara utakutana na mabonde, milima na wakati mwingine utalazimika kupita juu ya madaraja mabovu ya kuvuka mito yenye mamba na viboko!
Moja ya sababu zinazochangia kuvunja mahusiano ya kindoa ni USALITI. Kwanini usaliti unaingia kwenye ndoa ni mada nyingine tutakaoijadili wakati mwingine. Yatosha kusema kwamba wanawake wamekuwa jasiri sana kusimamia ndoa zao pale zinapokumbwa na dhoruba hii. Wanawake mara nyingi wanapogundua mume ana mahusiano nje ya ndoa hawaachii ngazi. Katika mazungumzo ya kawaida siyo ajabu ukasikia watu wanasema “huyu mwanamke sijui anangoja nini haondoki”. Swali hili ni pasua kichwa hasa kwa watu ambao hawajaonja tamu na chungu ya ndoa
Moja ya mambo ambayo hushtua wanandoa sana ni pale mmoja anapogundua kuwa mwenziwe kumbe siyo muaminifu kama alivyoaamini pale mwanzo! Makala hii itaangalia zaidi upande wa wanawake na jinsi wanavyochukulia kitendo cha kusalitiwa kwenye ndoa. Wakati naandika makala hii, nilijaribu kudodosa baadhi ya wanawake wa hali za maisha tofauti tofauti – kiuchumi, kielimu, kiimani za dini, kiumri pia. Nilichogundua ni kwamba wengi wa wanawake waliokaa kwenye ndoa zaidi ya miaka kumi, walishapitia misukosuko kadhaa ya kusalitiwa na waume zao. Wengine walisalitiwa na wanawake waliokuwa na uhusiano nao kwa namna moja au nyingine. Wapo waliokuwa na uhusiano kikazi – wasaidizi wa ndani, masekretari, wabia kibiashara n.k. Wengine walisalitiwa na wanawake waliokuwa ndugu au marafiki wa karibu sana.Vyovyote ilivyokuwa, tukio au matukio hayo yalileta uchungu mkubwa sana na kuzorotesha mahusiano ya ndoa. Kwa wengine matukio hayo yalileta “neema” kimaisha na hata katika uhusiano.
Kwa wanawake ambao ndoa zao zilikuwa changa zenye chini ya miaka mitano, baadhi walionyesha kutokuamini kuwa waume zao wanaweza kuwasaliti! Waliona kama ni jambo lisilowezekana kwa vile waliamini wanawatosheleza kwa kila hali.Wengine waliendelea kwa kuelekeza lawama kwa wanawake wenzao kuwa wanachangia mume kutoka nje kwa sababu mbalimbali ambazo sitazijadili kwenye makala hii. Cha ajabu, wanawake wale ambao walionekana kutokufurahia tena ndoa zao, hawakuonyesha dalili zozote za kutaka kuachana na waume zao. Baadhi ya sababu walizozitoa ni kama zifuatazo:
1. Hofu ya kuishi peke yao:
Wanawake walionyesha kuwa na hofu sana ya maisha ya upweke. “Mwanamke aliyeolewa akiwa na miaka 23, akakaa kwenye ndoa miaka 20 na kuendelea siyo rahisi sana kujikata na kuanzisha maisha ya peke yako”- ndivyo alivyosema mama Doris ( siyo jina lake halisi). Mama Doris aliolewa akiwa na umri wa miaka 23 akiwa bado chuoni. Hakuwahi kuishi peke yake.Aliishi na wazazi kabla ya kuolewa. Amekaa na mume zaidi ya miaka aliyoishi na wazazi wake. Ataanzaje maisha ya peke yake? Kwake ilimuwia vigumu sana kutoka na kwenda kuanza kuishi peke yake kwa vile hakua na uzoefu. Aidha alizidi kusema kwamba ataanzaje tena kuanza kutafuta mwenza mwingine katika umri ule?
2. Kuhofu kutokujimudu kifedha:
Kipato nacho huchangia sana kumfanya mwanamke aone vigumu kumwacha mwenza wake kisa amemsaliti kindoa. Mrs Y. alinitonya kwamba, kitendo cha mumewe kutoka nje ya ndoa pamoja na kumuumiza kisaikolojia, bado hakitoshi kumfanya aachane na mumewe. Mumewe ni mtu mkarimu sana kifedha na hicho nacho ni kichocheo cha tabia ya mume kutoka nje. “Wanawake wanajigongagonga sana kwa mumewe kwa sababu ya uchumi mzuri alio nao” alisema Mrs Y. Endapo ataondoka, ni kama kujiadhibu kwa sababu hizo pesa zitaliwa na hao mahawara kiulani zaidi. Pia yeye hana kipato kikubwa japo maisha yake ni ya hali ya juu sana. Haondoki ng’o!
3. Hakuna mwanaume aliye mkamilifu:
Wanawake wengi waliamini kwamba wanaume wote ni sawa utadhani wamezaliwa na baba mmoja mama mmoja! Usemi huu wa jumla na wenye maana nzito ulinifanya niwe mdadisi zaidi kutaka kujua unahusiana vipi na kuachana na mwanaume asiye mwaminifu? Mama “B” hakusita kuhitimisha na kusema “Wote wako sawa ila wanatofautiana viwango tu. Kadiri wanandoa wanavyoishi pamoja ndivyo polepole hugundua kuwa zile ndoto za mwanzo kuwa huyo ni wako peke yako hupungua na hata kutoweka baada ya muda”. Mama B ni mama mwenye watoto watano na wajukuu watatu. Ameolewa kwa miaka 35. Kipindi chote cha ndoa, ameishi na mume mwenye tabia ya kusaliti ndoa. Mumewe amezaa mara mbili nje ya ndoa na mmoja wa aliyezaa naye ni binti wa rafiki yake! Kasheshe lililotokea baada ya aibu hiyo sitaweza kuliandika hapa kwa sababu hakunipa ruhusa kuliandika. Ila yatosha kusema tu kuwa mama huyu mcheshi, mkarimu na mwenye upendo alimsamehe mumewe na kuendelea kuishi naye.
4. Kupoteza utambulisho:
Hili la utambulisho limenikumbusha kisa na mkasa wa marehemu Profesor Maathai Wangari na visa vya kulazimishwa aache kutumia jina la mumewe baada ya talaka!Hili ni janga kwa wanawake kama alivyosema Mrs L. Mhadhiri wa chuo kimoja maarufu. “Fikiria mwanamke uliyetambulika kama Mrs L maisha yako yote, ukajijengea utambulisho na sifa kwa kutumia jina la mume. Ghafla unatalikiana na mwenza wako na kulazimika kurudia jina lako la zamani, jina ambalo hakuna anayelijua isipokuwa walimu wako wa shule ya msingi na sekondari! Utakubali kupoteza kila kitu?” Siyo wengi wenye ujasiri kama wa marehemu profesa Maathai Wangari kwa kukomaa na kutumia akili ya ziada ya kuongeza herufi moja kwenye jina na kuonyesha kuwa hilo siyo jina la huyo mume anayeringa na jina kusudi tu amkomoe mke. Mwanamke aliyekwisha kujijengea jina kikazi au kibishara kwa kujulikana “Mrs” Fulani, humuwia vigumu kuanza kujenga tena sifa yake upya. Jina la mume hasa kama ni kubwa, ni mtaji mzuri kibiashara au kikazi. Mwanamke wa hivi, hawezi kumuacha mumewe kwa vile kamsaliti katika ndoa.
5. Hofu ya kupoteza marafiki:
Mwanamke aliyeolewa mara nyingi anajizolea heshima kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kwa msingi huu, atajitahidi sana kuchunga ndoa yake isisambaratike. Anajua kabisa kwamba atakapoanza kutafuta talaka na kuipata, kuna uwezekano mkubwa sana wa kupoteza marafiki kwa vile hao marafiki watamuona “siyo mwenzetu tena huyu”. Jamii nyingi huhusisha maisha ya upweke bila ndoa, kama maisha ya uhuru usio wa heshima. Hata binti anayeishi peke yake, humuwia vigumu sana kuaminiwa na vijana wa kiume kama binti mwenye wasifu wa kuweza kuoleka. Aghalabu huweza kumtumia tu kwa starehe japo wapo pia wasichana wenye kuishi peke yao wanaoolewa.
6. Familia kukataa kumkubalia atafute talaka:
Kiafrika mke na mume ni sehemu ya familia pana. Pamoja na kuwa na uwezo kisheria kufanya maamuzi yao wenyewe, bado kuna mambo ambayo lazima yapate Baraka ya familia pana ( extended family). Mke na mume huoana baada ya kupata “baraka” za namna moja ama nyingine kutoka kwa familia. Mchumba hutambulishwa na kukubalika, kisha familia nzima hushiriki kupanga harusi. Hii ina maana mke huyu ni kama “wa ukoo” au wa “familia” na pia mume naye huingia kuwa mmoja wa wana ndugu wa upande wa mke. Mke akipatikana na tatizo, jamii nyingi hushauri tatizo lipelekwe kwenye familia kupata ufumbuzi. Kwa maana hiyo, mke hawezi kukurupuka tu na kudai talaka bila kupitia ngazi mbalimbali za usuluhishi.Hata Sheria ya Ndoa ya 1971 ya Tanzania inataka wanandoa watafute usuluhisho kwanza kabla ya kupata kibali cha kufungua kesi ya talaka mahakamani.Mila nyingi za kiafrika ni kama haziruhusu talaka na ni kama vile talaka haipo! Kidini kadhalika, kuan madhehebu hairuhusu talaka hadi kifo kiwatenganishe.
7. Kuwekeza sana kwenye Hisia kwa mume:
Kuna wanawake hawawaachi waume zao kwa sababu tofauti sana. Hushindwa kuachana na mume kwa vile amewekeza sana maono ya moyoni kwa huyo mwanaume kiasi ambacho hushidwa kujikata kama mtoto aliyeshikiliwa na kitovu kwa mama.”Kumpenda mtu kwa moyo wako wote kwa muda mrefu hujenga mnyororo mgumu sana kiasi ambacho kufungua na kutokomea msionane tena ni kitu kigumu mno”. Ndivyo alivyoniambia Bi Sara (siyo jina halisi) Mwanamke kama huyu mara nyingi amejiweka katika hali ya kuishi maisha yake yote na huyo mume, amezaa na watoto ambao wameimarisha ule uhusiano ukawa zaidi ya undugu. Mume amekuwa zaidi ya ndugu zake wa damu. Kwa vyovyote itamuwia vigumu sana kuachana na mume huyu.
8. Kuwa na agenda ya siri
Wako wanawake ambao hata iweje, hawaachani kamwe na waume zao. Wao wanausoma mchezo mzima unavyokwenda wa kusaliti. Hata mwanaume asaliti mara mia, wao bado wako gado! Mwanamke kama huyu anaona mbali zaidi ya unavyoweza kufikiria. Ana malengo yake ya muda mfupi na mrefu tena yenye manufaa makubwa! Nani anaweza kujiuliza ni kwa vipi Hillary Clinton aliweza kusimama imara wakati wa kashfa ya ngono ya mumewe? Leo Hilary yuko wapi? Je angejikita kutafuta talaka ingemfikisha hapo alipo sasa? Kadhalika miongoni mwa jamii zetu za kitanzania, ni wanawake wangapi wa aina hiyo tunawajua? Huu ni mtihani nakuachia – noa bongo utabaini baadhi ya wanawake kama hawa.
10. Usaliti huweza kuimarisha ndoa.
Ndivyo ilivyoandikwa hujakosea ulichosoma. Wakati mwingine jambo ovu huweza kuzaa jema vilevile. Baada ya kosa la usaliti, Betty (siyo jina halisi) alijikuta akiwa karibu zaidi na mumewe. Waliafanya tathmini ya maisha yao, wakajadili mapungufu yao na kila mmoja akakubali kurekebisha kasoro zile. “Unjaua, kabla ya tukio, mawasiliano ni kama yalikwa yamekatika kwa miaka kadhaa. Kila mmoja alikuwa anaishi kivyake tu. Nilipopata ushahidi wa kilichokua kinaendelea, nilimuuliza. Kwa kweli ulitokea ugomvi mkubwa mno lakini tuliishia kulia pamoja na kuapa kuijenga upya ndoa yetu”. Ndivyo Betty na mumewe walivyofanikiwa kuokoa ndoa yao ya miaka 8
 
CHANZO: UJANATZ
Download Our App

1 comments:

Nimependa sana makala yako.Ninaamini itawasaidia sana wanandoa ktk kuboresha ndoa zao.

Reply

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top