Baada ya miezi mitatu ya mchuano mkali
hatimaye mshindi wa shindano la kuimba la Epiq Bongo Star Search atapatikana leo
katika fainali kali inayofanyika katika ukumbi wa Diamond
Jubilee.
Mshindi atajinyakulia shilingi milioni
hamsini pamoja na mkataba wa kurekodi kutoka kwa wadhamini pekee wa shindano
hilo kampuni ya simu za mikononi ya Zantel.
Washiriki walioingia kwenye fainali hizo ni
EBSS06: Nsami Nkwabi, EBSS07: Nshoma Ng’hangasamala, EBSS09: Salma Abushiri,
EBSS11: Wababa Mtuka (Dar) na EBSS12: Walter Chilambo
(Dar).
Wasanii watakaoburudisha ni Rich Mavoko,
Omi Dimpoz, Ben Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto,
Laila Rashid, Linex na Barnaba.
Akizungumzia fainali hizo, jaji mkuu wa
shindano hilo, Madam Ritha Paulsen, aliwashukuru watanzania kwa ushirikiano
waliowapa toka shindano limeanza mpaka leo wanahitimisha kwa
fainali.
‘Kama mlivyoona shindano hili toka
lilipoanza mwaka huu limekuwa la kimataifa zaidi, hivyo tarajieni fainali za
kipekee na zitakazoweka rekodi kwenye tasnia ya burudani na ni matarajio yetu
kwamba mshindi wa usiku huu atafanya vizuri kwenye muziki’ alisema Madam
Ritha.
Kwa upande wake Afsa Biashara mkuu wa
Zantel, bwana Sajid Khan alisisitiza utayari wa kampuni yake katika kuwaendeleza
vijana wa kitanzania kufikia ndoto zao lakini aliomba pia wadau wengine wa sanaa
kuwapa washirikiano washiriki wote.
‘Zantel, pamoja na kumpa mshindi zawadi ya
milioni hamsini lakini pia tutampa mkataba wa kurekodi, na washiriki wengine
watapewa nafasi ya kurekodi wimbo mmoja mmoja lakini juhudi hizi zitafanikiwa
ikiwa tutapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau’ alisema
Khan.
Shindano hilo limekuwa likirushwa hewani na
kituo cha runinga cha ITV, lilianza mwezi wa sita kwa kufanya usaili mikoani,
ambalo mwaka huu lilienda mikoa nane-Mbeya, Dodoma, Mwanza, Tanga, Dar es
Salaam, Zanzibar, Lindi pamoja na Arusha.
Kwa mara ya kwanza pia shindano hilo
liliweza kufanya usaili kwa njia ya simu ili kuwapa nafasi vijana zaidi ambao
hawakufikiwa na majaji.
Post a Comment