Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea ujumbe maalumu toka kwa Rais Ali Bongo wa Gabon uliowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko Maalumu wa Uwekezaji wa nchi hiyo Bw. Serge Mickoto Novemba 21, 2012 Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipitia ujumbe maalumu toka kwa Rais Ali Bongo wa Gabon Novemba 21, 2012 Ikulu jijini Dar es salaam uliowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko Maalumu wa Uwekezaji wa nchi hiyo Bw. Serge Mickoto Novemba 21, 2012 Ikulu jijini Dar es salaam.(PICHA NA IKULU).
Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon, zilizowasilishwa na Bw. Serge Mickoto.
Katika salamu hizo, Rais Bongo amemtaka Rais Kikwete kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali.
Rais Kikwete amemwambia mjumbe huyo wa Rais Bongo, kuwa Tanzania inathamini ushirikiano uliopo na juhudi za kuuendeleza ushirikiano huu ni muhimu kwa nchi zote mbili.
Mapema jana asubuhi Rais Kikwete alipokea hati za utambulisho za mabalozi kutoka Iran na Canada.
Wa kwanza kuwasilisha hati zake ni balozi Mehdi Agha Jafari na kufuatiwa na Balozi wa Canada Bw. Alexandre Leveque.
Mara baada ya kupokea hati zao Rais Kikwete amefanya mazungumzo na Mabalozi hao na kuwaeleza hali ya kisiasa na ushirikiano baina ya nchi zao na Tanzania.
Rais amemueleza Balozi wa Canada kuhusu mchakato wa Katiba unaoendelea nchini sasa hivi na kumueleza kuwa anatarajia kuwa nchi itapata Katiba itakayohakikisha nchi inabakia kuwa na Amani na Umoja.
“Tunataka kuhakikisha kuwa Umoja wa Kitaifa unabakia, hakuna migawanyiko ya kidini wala kikabila, tunataka Katiba ambayo haitaleta migawanyiko ya aina yeyote wala kupendelea kundi lolote nchini Mwetu” Rais amesisitiza.

“Mwisho”
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
IKULU
21 Novemba,2012