Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya ujio wa Rais Jakaya Kikwete kesho (04/11/2012) mkoani Singida.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
Rais wa jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Singida kuanzia kesho mchana (4/11/2012).
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone,alisema Rais Dkt. Kikwete atapokelewa saa sita mchana kesho akiwa anatokea mkoani Manyara.
Alisema baada ya kupokelewa,atapewa taarifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida,na shughuli hiyo itafanyikia kwenye Ikulu ndogo iliyopo mjini Singida.
“Baada ya kupewa taarifa hiyo,ataelekea kijiji cha Mwankoko kilichopo manispaa ya Singida ambapo ataweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji.Baada ya kuweka jiwe la msingi atazungumza na wananchi watakaokuwa wamekusanyika katika eneo hilo”,alisema na kuongeza.
“Mradi huu ni mkubwa kwani hadi utakapokamilika,utakuwa umegharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 19.7”.
Mkuu huyo wa mkoa,alisema kuwa siku inayofuata,Rais ataelekea Itigi wilaya ya Manyoni ambapo saa nne asubuhi,atazindua ujenzi wa barabara ya Manyoni- Itigi-Chaya yenye urefu wa kilometa 89.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
“Baada ya kazi hiyo ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo,saa 5.45 asubuhi,atafungua barabara ya Isuna- Manyoni yenye urefu wa kilometa 54 iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa thamani ya shilingi bilioni 32.Pia atazungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika eneo hilo la ufunguzi wa barabara”alisema Dk.Kone.
Alisema baada ya hapo, Rais Kikwete ataondoka kuelekea Dodoma mjini kwa majukumu mengine.
Post a Comment