KATIBU wa Bunge Dk.
Thomas Kashililah, amesema kuwa taarifa kuhusu ripoti ya kamati ndogo iliyoundwa
kuchunguza tuhuma za wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa, itawasilishwa
bungeni siku yoyote kuanzia leo katika mkutano unaoendelea
sasa.
Dk. Kashililah aliyasema
hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili, akitakiwa kufafanua kuhusiana na
ripoti hiyo na kile kinachoaminika kuwa ni msimamo wa Spika Anne Makinda,
kutotaka ripoti hiyo isisomwe bungeni.
“Kwa mujibu wa Sheria ya
296 inayohusu Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge hili jambo linahusu haki, ni
lazima taarifa yake itawasilishwa,” alisisitiza Dk. Kashililah.
Hata hivyo, licha ya
kulihakikishia gazeti hili kuwa ripoti hiyo itawasilishwa bungeni lakini
alikataa kutaja ni siku husika na kusisitiza kuwa tayari Spika amekwishaifanyia
kazi.
Dk. Kashililah alisema
Spika hajaing’ang’ania ripoti hiyo kama ambavyo wengi wamekuwa wakiamini na
kwamba uamuzi wowote utakaofanywa kuhusu ripoti hiyo utakuwa ni wa
wazi.
Alisema baada ya Spika
kuifanyia kazi ripoti hiyo, ataamua kama yeye aiwasilishe au airudishe kwenye
kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Brigedia Hassan Ngwilizi, itoe
taarifa.
Kuhusu taarifa ya ripoti
hiyo kutokuwamo kwenye ratiba za shughuli za Bunge, Dk. Kashililah alisema hilo
halimzuii Spika kupanga utaratibu wake wa kuipeleka bungeni.
“Spika anapotaka
kuliingiza jambo kwenye shughuli za Bunge hahitaji kuliweka katika ratiba,
atakapoamua itaingizwa kwenye Order Paper (ratiba inayoonyesha shughuli za Bunge
kwa siku)…mamlaka anayo, anaweza kurekebisha,” alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya
mkutano wa tisa wa Bunge, leo baada ya kipindi cha maswali na majibu,
utawasilishwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka
2012.
Kesho baada ya kipindi
cha maswali, kutakuwa na tathmini ya matumizi ya Kanuni za Kudumu za Bunge siku
ambayo pia huenda suala la taarifa ya ripoti hiyo ya Ngwilizi ikaingizwa kwenye
ratiba.
Alhamisi ratiba
inaonyesha kuwa kutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu na baada ya hapo, yatafuata
maswali ya kawaida kisha hoja binafsi za wabunge na Ijumaa baada ya maswali
kutakuwa na hoja binafsi za wabunge kabla ya kuahirisha Bunge.
Tangu kamati ya Ngwilizi
imalize uchunguzi wake na kukabidhi ripoti kwa Spika, kumekuwepo na taarifa
kadhaa zikidai kuwa Makinda anakataa ripoti hiyo isijadiliwe kwa maelezo kuwa
anahitaji muda kuifanyia kazi.
Makinda alitoa uamuzi
wakati wa kikao cha wabunge wote kilichokuwa kikijadili ratiba ya shughuli za
Bunge hili la tisa.
Bila kutoa ufafanuzi wa
kina, Spika Makinda alisema yeye ndiye anajua lini na wakati gani wa kuileta
hoja hiyo bungeni na kamwe hawezi kuileta kwa shinikizo la
wabunge.
Hata hivyo, hatua hiyo
iliibua maswali kutoka kwa baadhi ya wabunge waliotaka kujua sababu za kutoileta
ripoti hiyo ijadiliwe bungeni, lakini Spika hakutaka kutoa ufafanuzi na badala
yake alisisitiza kwamba haitajadiliwa katika mkutano huo wa
Bunge.
Makinda anaelezwa kuwa
asingeweza kuileta ripoti hiyo bungeni kwani uchunguzi umebaini hakuna mbunge
aliyejihusisha na rushwa wakati tayari alishavunja Kamati ya Nishati na Madini
kwa tuhuma hizo.
Wajumbe wengine waliomo
kwenye kamati ya Ngwilizi ambaye pia ni mbunge wa Mlalo ni Saidi Arfi (Mpanda
Kati), John Chiligati (Manyoni Mashariki), Goesbert Blandes (Karagwe) na Riziki
Omary Juma (Viti Maalumu).
Lipumba
ambana
Wakati huo huo Spika
Makinda ameendelea kung’ang’aniwa akitakiwa kuwasilisha mbele ya Bunge ripoti ya
uchunguzi wa tuhuma za wabunge kudaiwa kupokea rushwa.
Akizungumza na Tanzania
Daima jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba, alisema hatua ya kukalia ripoti hiyo inaudhalilisha muhimili
huo na kamati iliyofanya kazi hiyo.
Prof. Lipumba alisema
kuwa ni muhimu Watanzania wakatoa shinikizo ili kiongozi huyo aiweke ripoti hiyo
hadharani kuliko kuendelea kubaki nayo na kuiweka kabatini.
“Kitendo cha kubaki nayo
bila kuiweka mezani kwanza, kinalidhalilisha Bunge pili anataka kuufanya mjadala
huo kuwa mrefu zaidi jambo ambalo halipendezi,” alisema.
Alisema kuwa hata
kiongozi huyo akiendelea kubaki nayo anapaswa kufahamu kuwa ripoti hiyo
imeandaliwa na watu hivyo inaweza kuendelea kuvuja
vipandevipande.
Prof. Lipumba alisema
kuwa iwapo Makinda atashindwa kuleta ripoti hiyo kwa wakati kuna uwezekano wa
kuonekana kuwa imebadilishwa tofauti na ile iliyoandaliwa na kamati
husika.
Alisema kuwa Spika
Makinda anapaswa kuwa tayari kuitoa ripoti hiyo hata kama itakuwa inaiumiza
serikaki na washirika wake kwa kuwa huo ndiyo uwazi na demokrasia
kukua.
Post a Comment